2015-07-16 14:40:00

Waelimisheni vijana kwa kuwainjilisha na kusikiliza kilio chao cha ndani!


Jubilei ya miaka 200 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Bosco, iwe ni fursa kwa Wasalesiani wa Don Bosco kushikamana na vijana kwa ajili ya utume kwa vijana. Ni nafasi ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya Mtakatifu Yohane Bosco, mtume wa vijana, mwaliko na changamoto ya kuambata urithi wa maisha ya kiroho na shughuli za kichungaji zilizoachwa na Mtakatifu Yohane Bosco, ili kuweza kuzimwilisha kwa ujasiri.

Huu ni muhtasari wa barua kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko aliyomwandikia Mheshimiwa Padre Angel FernĂ ndes Artime, Mkuu wa Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco wanaposherehekea Jubilei ya miaka 200 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Bosco, mlezi na mchungaji mwema wa vijana na kwamba, karama ya Roho Mtakatifu aliyolikirimia Shirika imekuwa ni zawadi kubwa kwa Mama Kanisa katika nyakati hizi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya miaka 200 ya kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Bosco, alipata bahati kukutana na kuzungumza na Familia ya Mtakatifu Yohane Bosco katika Kanisa kuu la Bikira Maria msaada wa Wakristo, mahali ambamo masalia ya Mtakatifu Yohane Bosco yamehifadhiwa.

Baba Mtakatifu anaitaka familia ya Mtakatifu Yohane Bosco kutoka kimasomaso kwa ajili ya utume kwa vijana, ili waweze kuambata maisha; kukutana na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao pamoja na kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha yaani: hali ya kukata tamaa; Kwashakoo ya maisha ya kiroho pamoja na kutengwa.

Wasalesiani wawe ni mfano bora wa kuigwa katika kuwashirikisha vijana mang’amuzi ya elimu na malezi yanayogusa maisha ya mtu mzima; kwa kuwapatia fursa ya elimu na ujuzi; daima wakitafuta ustawi, maendeleo na mafao ya mtu mzima. Wawasaidie vijana kujenga moyo wa sala na kazi, kwani mchakato wa Uinjilishaji na elimu ni chanda na pete; waelimishe kwa kuinjilisha na kuinjilisha kwa kuelimisha.

Wawaonjeshe vijana upendo kwa kushiriki katika maisha na mahangaiko yao, ili kuwapatia majiundo makini katika hija ya maisha. Wawaundie mazingira ya kifamilia, kwa wao kuwa kama: baba, mwalimu na rafiki wa vijana, ili kuwaonjesha furaha inayobubujika kutoka katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Kwa njia ya upendo thabiti, vijana wanaweza kufanya maamuzi makini katika maisha yao. Wasalesiani wajisadake bila kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia vijana maskini bila ubaguzi kwa kuendelea kujikita katika ari na mwamko wa kimissionari pamoja na kushirikiana na waamini walei, ili kutekeleza dhamana hii.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mtakatifu Yohane Bosco alionesha huruma kwa kujikita katika wokovu wa vijana, akamshuhudia Kristo, akatangaza Injili kwa moyo mkuu na kuonesha umoja na Kanisa pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Alikuwa ni mtu wa sala na Ibada ya pekee kwa Bikira Maria, akabahatika kutenda miujiza miongoni mwa vijana.

Leo hii, Familia ya Wasalesiani inakabiliwa na changamoto ya elimu na kimissionari hali inayojionesha kwa watu wa dini mbali mbali, katika nchi zinazoendelea duniani na hata katika maeneo ambayo kuna wimbi kubwa la wahamiaji. Uchu wa mali na madaraka; ukosefu wa haki na usawa; ukoloni mamboleo na changamoto za ukuaji wa miji ni kati ya mambo ambayo vijana wanakumbana nayo kwa wakati huu. Matumizi ya mitandao ya kijamii na vyombo vya mawasiliano ya kijamii ni kati ya mambo yanayowagusa vijana kwa karibu zaidi, kiasi hata cha kuwasababishia mkanganyiko katika maisha.

Baba Mtakatifu anaialika Familia ya Wasalesiani kujifunga kibwebwe ili kupambana na changamoto hizi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa vijana wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; vijana waliojeruhiwa katika malezi na makuzi yao; vijana ambao hawakupata nafasi ya kusikilizwa kwa makini; wote hawa wanapaswa kusindikizwa na kusaidiwa ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda amini wa Kristo kati ya watu wanaowazunguka.

Vijana wana kiu ya maisha; uhuru na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Wasaidiwe kujenga na kudumisha ulimwengu unaojikita katika haki na udugu; ustawi na maendeleo ya wengi; utunzaji bora wa mazingira na kanuni za maisha. Kwa njia hii vijana wanaweza kuwa kweli ni marafiki amini wa Yesu, tayari kusindikizwa katika mchakato wa maisha ya imani, huku wakiambata Injili ya maisha na kusimama kidete kulinda na kutetea mambo msingi katika maisha.

Baba Mtakatifu anaitaka Familia ya Wasalesiani kuwafunda vijana utu mintarafu uelewa wa Kikristo; kwa kutumia lugha mpya ya njia za mawasiliano ya jamii, ili waweze kupata picha kamili ya binadamu na maisha ya kidini; tayari kujisadaka pia kwa ajili ya kuwasaidia jirani zao; kwa kuheshimu utu wa binadamu na thamani ya kazi ambayo kimsingi ni utimilifu wa binadamu.

Wasalesiani wawe ni Wainjilishaji na waelimishaji; wasomi na watu wa sala; ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika mfumo wa elimu mamboleo. Wasalesiani wawe tayari kushirikiana na kushikamana na wadau mbali mbali katika sekta ya elimu, ili kusaidia kuwafunda vijana duniani kote. Dhamana hii waitekeleze kwa kukazia utume wa familia.

Vijana watambue kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa na Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu, ili kuwaokomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Wasalesiani waendelee kujikita pia katika utoaji wa katekesi makini kwa vijana kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; unaoambata Neno la Mungu, Maisha ya Kisakramenti na Ibada kwa Bikira Maria. Wawe ni mashuhuda wa Injili ya furaha na mapendo; tayari kuendeleza karama ya Mtakatifu Yohane Bosco kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya vijana: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.