2015-07-14 11:09:00

Salam na matashi mema kwa wakuu wa nchi kutoka kwa Papa Francisko


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 13 Julai 2015 amerejea mjini Vatican baada ya kuhitimisha hija yake ya kitume Amerika ya Kusini kwa kutembelea Equador, Bolivia na Paraguay. Hii ni hija ambayo imeacha chapa na mwaliko wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Furaha kwa kujikita katika ari na mwamko wa kimissionari; tayari kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha.

Baba Mtakatifu akiwa njiani kurejea mjini Vatican ametuma salam na matashi mema kwa wakuu wa nchi za: Paraguay. Bolivia, Brazil, Cape Verde, Moroco, Hispania na Italia. Baba Mtakatifu amewaombea: amani, furaha na matumaini; umoja, mshikamano, ustawi na maendeleo ya watu wao pamoja na kuwapatia baraka zake za kitume.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Rais Sergio Mattarella wa Italia anakaza kusema, akiwa Amerika ya Kusini, amebahatika kukutana na kuzungumza na bahari ya waamini na watu wenye mapenzi mema. Waamini wanaonesha ari na mwamko wa kutaka kukua na kuendelea kukomaa katika imani na maendeleo endelevu. Amewahakikishia wananchi wa Italia sala zake kwa ajili ya mafao ya wengi, utulivu na maendeleo kwa wananchi wote wa Italia.

Baba Mtakatifu alipowasili mjini Roma, alikwenda moja kwa moja kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma, kumshukuru Bikira Maria kwa ulinzi na tunza yake ya kimama. Baba Mtakatifu ameweka shada la maua mbele ya Sanamu ya Bikira Maria kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.