2015-07-07 11:00:00

Kanisa Amerika ya Kusini linataka kujikita katika mchakato wa Umissionari!


Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume Amerika ya Kusini, kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 13 Julai 2015 anaendelea kukazia umuhimu wa kuthamini tofauti zinazojitokeza miongoni mwa watu kama utajiri mkubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Anawahimiza viongozi wa jamii kuhakikisha kwamba, wanawashirikisha watu katika kupanga na kutekeleza maamuzi mbali mbali katika maisha yao sanjari na kuendeleza majadiliano yanayolenga mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu.

Ni wajibu wa jamii kuwalinda na kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kwamba, Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa na Mama Kanisa kusimama kidete kulinda, kutetea na kutangaza Injili ya Famialia inayojikita katika Injili ya Uhai ambao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni changamoto ya kukataa utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba.

Professa Guzman Carriquiri, Katibu mkuu wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini ambaye yuko kwenye msafara wa Baba Mtakatifu Francisko wakati huu huko Amerika ya Kusini anasema kwamba, Baba Mtakatifu kwa sasa anatembelea nchi tatu ambazo zinaendelea kuibukia katika maendeleo. Katika kipindi cha miaka kumi na miwili, nchi ya Equador, Bolivia na Paraguay zimeendelea kukua na kupanuka katika masuala ya uchumi na maendeleo ya watu. Takwimu za ukuaji wa kiuchumi zinazonesha kwamba, uchumi unakua kwa asilimia 5% kila mwaka.

Licha ya mafanikio haya Professa Guzman Carriquiri anakiri kwamba, bado kuna kundi kubwa la maskini; kuna mipasuko ya kijamii kutokana na ukosefu wa usawa kati ya watu; utawala wa mabavu kwani hapa kwa sasa demokrasia na utawala shirikishi ndio kwanza unaanza kushika kasi. Kanisa alilolikuta wakati Mtakatifu Yohane Paulo II alipokuwa anafanya hija ya kichungaji Amerika ya Kusini, miaka thelathini iliyopita, limebadilika, kwani ulikuwa ni wakati wa taalimungu ya ukombozi.

Leo hii Kanisa limeshikamana katika umoja, linaendelea kutekeleza sera na mikakati iliyotolewa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, Aparecida, ujumbe uliomwilishwa kwa kiasi kikubwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume, Injili ya Furaha, “Evangelii gaudium” . Nyaraka hizi mbili ni ufunguo wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Amerika ya Kusini.

Hapa Kanisa halina budi kujielekeza zaidi katika kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimissionari; tayari kuwashirikisha watu Furaha ya Injili, imani na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Huruma na upendo wa Mungu ni ujumbe unaowakumbatia wote na wala hakuna mtu awaye yote anayeweza kutengwa. Kanisa linataka kuwaonesha wema na huruma ya Mungu kwa njia ya huduma makini.

Waamini wanahamasishwa kuwa mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo sanjari na kuendeleza mchakato wa utamadunisho, ili kweli imani iweze kuwa ni sehemu ya vinasaba na vipaumbele vya waamini wa Amerika ya Kusini. Baba Mtakatifu Francisko anataka kuwasaidia waamini kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria; kuonesha upendo na mshikamano na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani hawa ni amana ya Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji mpya.

Professa Guzman Carriquiri anasema, Baba Mtakatifu akiwa nchini Equador atatembelea gereza kuu la Santa Cruz de la Sierra, hili ni kati ya magereza hatari sana Amerika ya Kusini, hapo Baba Mtakatifu anataka kuwapatia wafungwa hawa matumaini mapya katika hija ya maisha yao. Baba Mtakatifu anataka kuwatembelea na kuwafariji watoto na wagonjwa; wazee na watu pweke, ili wote waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.