2015-06-30 08:28:00

Wanasiasa wanayo dhamana ya kutunga sera zinazodhibiti uchumi na fedha!


Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko juu ya utunzaji bora wa mazingira “Laudato si”, yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” umetolewa kwa wakati muafaka ili kuisadia Jumuiya ya Kimataifa kuweza kukabiliana na changamoto kubwa zinazotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Ni matumaini ya Vatican kwamba, Waraka huu ukijadiliwa katika ukweli na uwazi, itaiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kupata matunda yanayokusudiwa kwa kuhakikisha kwamba, binadamu anapewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya kimataifa.

Haya yamesemwa na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, Jumatatu, tarehe 29 Juni 2015 wakati alipokuwa anashiriki mkutano wa ngazi ya juu kabisa wa viongozi wa Umoja wa Mataifa, huko New York, Marekani. Mkutano wa Rio de Janeiro uliofanyika kunako mwaka 1992, ulibainisha pamoja na mambo mengine kwamba, binadamu anapaswa kuwa ni kiini cha sera na mikakati ya maendeleo endelevu kwa siku za usoni.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka huu anakaza kusema, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, wapewe msukumo wa pekee na Jumuiya ya Kimataifa, kwani hawa ndio waathirika wakubwa wa athari za mabadiliko ya tabianchi sehemu mbali mbali za dunia. Wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa wanahamasishwa kuambata ekolojia inayojikita katika utunzaji bora wa mazingira kwa ajili ya mafao ya wengi.

Umoja wa Mataifa katika mikutano mbali mbali umeonesha matokeo ya tafiti kuhusu mazingira, jambo la msingi kwa wakati huu ni kuhakikisha kwamba, matokeo ya tafiti hizi yanagusa watu husika, kwa kuangalia mateso na mahangaiko ya maskini duniani. Athari za mabadiliko ya tabianchi ni tatizo na changamoto za kimataifa inayogusa kwa namna ya pekee: mazingira, jamii, uchumi na siasa pamoja na ugawavi wa bidhaa, lakini athari zake zinatofautiana kutoka katika jamii moja hadi nyingine, changamoto ya kushirikiana na kushikimana ili kutafuta suluhu ya kudumu.

Baba Mtakatifu Francisko katika waraka wake juu ya utunzaji bora wa mazingira anasema kwamba, mazingira ni kwa ajili ya mafao ya wengi, lakini Jumuiya ya binadamu inaendelea kushuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira ambao haujawahi kutendeka kwa miongo kadhaa iliyopita. Hapa kuna haja ya kufanya mabadiliko makubwa katika mtindo wa maisha, uzalishaji na ulaji. 

Baba Mtakatifu pia anatoa ushauri wa jinsi ya kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inatoa sera na mikakati makini ya kupunguza na hatimaye, kudhibiti uzalishaji wa hewa ya ukaa na kuanza kutumia nishati rafiki kwa maendeleo na ustawi wa binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi pia kujifunga kibwebwe kupambana na baa la umaskini, kwa kujikita katika sera bora za utunzaji wa mazingira kwa kudhibiti mikakati ya maendeleo, uzalishaji, biashara na ulaji.

Tatizo si ukuaji na maendeleo ya sayansi na teknolojia, bali watu kuwa na ujasiri wa kubadili akili na mioyo yao; maamuzi pamoja na mapambano dhidi ya baa la umaskini unaoendelea kunyanyasa utu na heshima ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa iwe na mikakati makini katika udhibiti wa uchafuzi wa mazingira pamoja na vikolezo vya maendeleo kwa maskini.

Mambo haya anasema Kardinali Peter Turkson yanahitaji ujasiri katika kufanya mabadiliko, ili kuelewa mikakati ya uchumi na maendeleo. Siasa irejeshe demokrasia katika udhibiti wa uchumi na fedha; mambo msingi katika Jamii ya mwanadamu. Hii ndiyo njia nyofu inayopaswa kufuatwa na Jumuiya ya Kimataifa wakati wa mkutano wa Kimataifa wa athari za mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika mwezi Desemba, Paris, Ufaransa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.