2015-06-30 10:06:00

Ukristo unapata chimbuko lake katika dini ya Kiyahudi!


Roma ni mji ambamo wamezikwa Mitume Petro na Paulo, miamba wa imani na kwamba, mjini Roma ni mahali ambapo kunapatikana Jumuiya ya zamani kabisa ya Wayahudi, kielelezo makini kwamba, Wayahudi na Wakristo wamekuwa wakiishi kwa pamoja kwa takribani miaka elfu mbili iliyopita, ingawa mahusiano haya yametikiswa kwa kinzani na migawanyiko ya kidini.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican waliliona hilo na kuanzisha mchakato wa majadiliano ya kidugu kati ya Wakatoliki na Wayahudi, kama inavyobainishwa na Waraka wa Majadiliano ya kidini, Nostra aetate unaokazia kwamba, Ukristo unapata msingi wake kutoka katika dini ya Kiyahudi na kwamba, hakuna tena sababu ya madhulumu dhidi ya Wayahudi. Miaka hamsini ya majadiliano kati ya Wayahudi  na Wakatoliki imeleta mafanikio makubwa kwa kukazia urafiki na maelewano mazuri, kwani Roho Mtakatifu amesindikiza juhudi za majadiliano haya ya kidini.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe  30 Juni 2015 kwa wajumbe wanaohudhuria kongamano la kimataifa kati ya Wakristo na Wayahudi, lililoandaliwa na Baraza la Wakristo na Wayahudi Kimataifa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, udhaifu wa kibinadamu, kinzani na misigano; kiburi na majivuno; vimeshindwa kwa Roho ya Mungu mwenye nguvu, kiasi cha kusaidia kukuza imani na udugu, kiasi cha kuwa kweli ni marafiki na ndugu na wale si wageni; waamini wanaoungama imani kwa Mungu mmoja, Muumbaji wa dunia na Bwana wa historia. Ni wema na hekima ya Mungu inayotoa baraka katika mchakato wa majadiliano.

Baba Mtakatifu anasema, Wakristo wote wanapata chimbuko lao katika dini ya Kiyahudi ndiyo maana Baraza la Wakristo na Wayahudi Kimataifa, tangu mwanzo, limewakusanya Wakristo wa madhehebu mbali mbali, chini ya mwamvuli wa Kiyahudi. Wakristo wote wanaunganishwa na Kristo; Wayahudi umoja wao unajikita katika Sheria, Torah. Wakristo wanakiri na kuungama kwamba, Yesu Kristo, ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kwa Wayahudi, Neno la Mungu limesheheni katika Sheria.

Waamini wa dini zote mbili wanakiri na kumuungama Mwenyezi Mungu, mmoja na chanzo cha Agano, anayeendelea kujifunua kwa binadamu kwa njia ya Neno lake na hivyo kuwa kweli ni chemchemi ya maisha mapya. Haya ndiyo mambo msingi yanayobainishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Waraka wao juu ya Majadililiano ya kidini; mambo yanayoweza kuendelezwa zaidi anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika tafakari yao kuhusu dini ya Kiyahudi, walijikita katika mambo makuu kumi yaliyofafanuliwa kwenye mkutano wa Seeliserg, Uswiss, kunako mwaka 1947. Huu ukawa ni mwanzo wa Baraza la Wakristo na Wayahudi Kimataifa; cheche za ushirikiano na Kanisa Katoliki, zilizokuzwa na kuendelezwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Kunako mwaka 1974, Kanisa Katoliki likaanzisha Tume ya uhusiano wa kidini na Wayahudi.

Tume hii inaendelea kufuatilia kwa ukaribu zaidi shughuli mbali mbali zinazotekelezwa na Baraza la Wakristo na Wayahudi Kimataifa, katika mchakato wa majadiliano ya kidini. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawatakia heri na mafanikio mema washiriki wote wa Kongamano la Wakristo na Wayahudi Kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.