2015-06-30 09:05:00

Ugeni mzito unatembelea Jimbo Katoliki la Nyahururu, Kenya!


Patriaki Francesco Moraglia wa Jimbo kuu la Venezia, kuanzia tarehe Mosi Julai hadi tarehe 6 Julai 2015 kwa mara ya kwanza anatarajiwa kufanya hija ya kichungaji nchini Kenya kwa kutembelea kwenye Parokia ya Ol Moran, iliyoko Jimbo Katoliki la Nyahururu linaloongozwa na Askofu Joseph Mbatia. Parokia hii imeanzishwa na Padre Giacomo Basso kutoka Venezia. Patriaki Moraglia anaongoza ujumbe wa watu watatu kutoka Venezia.

Akiwa Jimboni Nyahururu, Patriaki Moraglia na ujumbe wake watatembelea Hospitali ya Jimbo iliyoko Kinangop; Uaskofuni na kituo cha maendeleo ya jamii cha Mtakatifu Martin. Watapata pia nafasi ya kuangalia maisha na utume wa Jimbo la Nyahururu, katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaopania kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili. Watatembelea vituo vya afya, elimu pamoja na kusali na Jumuiya ya shule ya msingi ya “Tumaini Academy.

Hapa Patriaki Moraglia anatarajiwa kubariki jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mapya. Atatembelea na kuangalia shughuli za Uinjilishaji zinazotekelezwa kwenye eneo la Mtakatifu Yohane wa XXIII. Hili ni eneo ambalo kwa mara ya kwanza katika historia ya Jimbo la Nyahururu limebahatika kutangaziwa Habari Njema ya Wokovu.

Patriaki Moraglia atakutana na kuzungumza na waamini wanaoanza kujenga msingi wa imani ya Kikristo katika maisha yao. Eneo hili limepewa kipaumbele cha pekee, kwani mchakato wa Uinjilishaji unakwenda sanjari na utoaji wa elimu na katekesi makini, ili kuimarisha misingi ya imani ya Kanisa Katoliki inayojikita katika: Kanuni ya Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala, kama inavyofafanuliwa na Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki. Patriaki Moraglia na ujumbe wake, watakutana na kuzungumza na Halmashauri walei, Makatekista pamoja na watawa wanaotoa huduma Parokiani hapo.

Patriaki Moraglia, hapo Jumapili tarehe 5 Julai 2015, anatarajiwa kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu kwenye eneo la Mtakatifu Karol Lwanga, Shahidi wa Uganda. Familia ya Mungu Ol Moran, itakusanyika ili kuendelea kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani kwa kuwapatia Kanisa Jipya la Parokia, ambalo lilitabarukiwa mwezi mmoja uliopita.

Jioni, akiwa Nyahururu, Patriaki Francesco Moraglia atakutana na kuzungumza na Mapadre wa zawadi ya Imani, “Fidei Donum” wanaotekeleza utume wao Jimboni Nyahururu. Atahitimisha hija yake kwa kukutana na kuzungumza na Askofu Joseph Mbatia wa Jimbo Katoliki la Nyahururu pamoja na kuadhimisha naye Ibada ya Misa takatifu. Tarehe 7 Julai 2015, Patriaki Francesco Moraglia atakuwa anarejea tena Venezia, ili kuendelea na shughuli na maisha yake ya kitume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.