2015-06-30 11:29:00

Papa Francisko anakwenda nchini Cuba kama Mmissionari wa huruma ya Mungu


Baraza la Maaskofu Katoliki Cuba, linapenda kumtolea Mwenyezi Mungu sifa na shukrani kwa kuijalia tena Familia ya Mungu nchini kukutana na Khalifa wa Mtakatifu Petro, baada ya kukutana na Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI na sasa Papa Francisko, atakayewatembelea kuanzia tarehe 19 hadi 22 Septemba 2015.

Hii ni hija ya kitume inayojikita katika matumaini na inakuja wakati muafaka kabisa, wakati Familia ya Mungu nchini Cuba inapoendelea kujikita katika mchakato wa upatanisho na amani kati ya watu; mambo ambayo yanapewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake. Baraza la Maaskofu Katoliki Cuba katika ujumbe wake kwa Familia ya Mungu nchini humo, linapenda kukazia umuhimu wa hija hii inayofanyika katika kipindi cha miaka kumi na saba.

Ni Cuba na Brazil peke yake ndizo nchi za Amerika ya Kusini zilizobahatika kutembelewa na Mapapa watatu. Kunako mwaka 1998 Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea Cuba, wakati ambapo nchi hiyo ilikuwa bado imetikiswa na athari za mapinduzi, akawa ni Papa wa kwanza kutembelea nchini Cuba kama mjumbe wa ukweli na matumaini. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alitembelea Cuba kama mjumbe wa upendo na Papa Francisko atatembelea Cuba kama Mmissionari wa huruma ya Mungu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Cuba linakaza kusema, walimwengu wanahitaji kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu, changamoto kwa Familia ya Mungu nchini Cuba kuhakikisha kwamba, inajiandaa kikamilifu ili kumpokea na kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko. Kama sehemu ya maandalizi haya, waamini wanatakiwa kujiandaa kwa maisha ya kiroho. Kila Ijumaa ya kwanza ya mwezi, waamini watakuwa wanasali kwa ajili ya kuomba huruma ya Mungu.

Wakati wa mkesha wa ujio wa Baba Mtakatifu Francisko, yaani kati ya tarehe 17 na tarehe 18 Septemba, kutafanyika mkesha wa sala, ili kuomba msaada na tunza ya Mungu, ili kweli Familia ya Mungu nchini Cuba, iweze kumsikiliza na kukumbatia ujumbe wa matumaini na huruma utakaowasilishwa kwao na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.