2015-06-30 15:19:00

Jengeni utamaduni wa ukarimu, epukeni ubinafsi na uchoyo!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, CCEE kuanzia tarehe 29 hadi tarehe 2 Julai 2015 linafanya mkutano unaowashirikisha wakurugenzi wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji na wakimbizi. Mkutano huu unafanyika huko Vilnius, Lithuania.

Lengo ni kujadili jinsi ya kumwilisha mshikamano wa upendo kwa njia ya huduma makini kwa wahamiaji na wageni ambao kwa sasa wanaonekana kuwa kero kubwa kwa mataifa mengi ya Ulaya. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya linakazia umuhimu wa kuheshimu na kuthamini utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Kwa bahati mbaya, wahamiaji na wakimbizi wamekuwa ni wahanga wakubwa wa biashara haramu ya binadamu, kiasi kwamba, wamegeuzwa kuwa kama bidhaa na vifo vyao huko Bahari ya Mediterrania na Jangwani, hakuna tena anayesikitika wala kuomboleza kutokana na vifo hivyo! Machozi ya wahamiaji na wakimbizi yamebaki majini kama “kilio cha samaki”.

Kardinali Josip Bozanic, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Zagabria, Mwenyekiti wa Idara ya wahamiaji, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huu, huko Vilnius anasema kwamba, Jumuiya ya Ulaya inaonekana kana kwamba, imechanganyikiwa na kugawanyika kuhusiana na changamoto ya wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta hifadhi Barani Ulaya.

Ni Jumuiya ambayo imekosa utamaduni wa ukarimu na mshikamano kwa  wahamiaji na wakimbizi ambao wanalazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na sababu mbali mbali. Viongozi wa Serikali wanayodhamana na wajibu wa kuwasaidia wahamiaji na wakimbizi ili kupata haki zao msingi badala ya nchi za Ulaya kuendelea kugubikwa na ubinafsi pamoja na uchoyo. Watambue kwamba, hawa ni watu wenye heshima na adhi yao na wala si mzigo wa kuwekwa kando.

Ukarimu unapania kujenga madaraja ya watu kukutana, kuheshimiana na kusaidiana kwa hali na mali. Ukarimu ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa, changamoto kwa Jumuiya za Kikristo kuhakikisha kwamba, zinajenga utamaduni wa ukarimu unaojikita katika uvumilivu na upendo. Kardinali Josip Bozanic anasema, changamoto ya ukarimu kwa wahamiaji ni changamoto endelevu inayopania kuwaonjesha watu wenye shida na mahangaiko huruma na upendo wa Mungu,

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.