2015-06-29 15:21:00

Vijana msitafute mafanikio ya haraka kwa njia ya mkato!


Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde wa Jimbo kuu la Mombasa, Kenya katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, Sherehe ya Mitume Petro na Paulo miamba wa imani inayoadhimishwa na Mama Kanisa tarehe 29 Juni ya kila mwaka, ni changamoto kwa waamini kulinda, kudumisha na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kama walivyofanya, Mitume Petro na Paulo, miamba wa imani, kiasi hata cha kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Hii ni siku ambayo Maaskofu wakuu wapya walioteuliwa katika kipindi cha mwaka mzima, wanasali na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa pamoja na Baba Mtakatifu kama kielelezo cha umoja na mshikamano wa imani, matumaini na mapendo na Kanisa zima. Maaskofu wakuu wapya wamepewa Pallio Takatifu alama ya Kristo mchungaji mwema anayewabeba Kondoo wake mabegani mwake, tayari kuwaongoza pole pole katika malisho ya majani mabichi, kando ya maji yenye utulivu. Mwaliko kwa Maaskofu wakuu kuwa pia ni kielelezo cha wachungaji wema na watakatifu kwa Kondoo wa Kristo.

Askofu mkuu Musonde anabainisha kwamba, Kanisa Barani Afrika limebahatika kuwa na idadi kubwa ya miito mitakatifu, jambo ambalo ni la kumshukuru Mungu na mwaliko wa kuwa na mwelekeo mpana zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji mpya kwa kusaidia Makanisa makongwe ambayo kwa sasa yanakumbana na ukata wa rasilimali watu, ili kuendeleza kazi ya Uinjilishaji. Kanisa Barani Afrika hata katika uchanga wake, linaonesha ukomavu na ushuhuda wa imani na maadili, changamoto kwa Wakristo kutokubali kuyumbishwa na malimwengu pamoja na ukanimungu.

Kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mombasa, anakabiliwa na changamoto kubwa ya kuwa na kundi ambalo lina ogelea katika umaskini, ukosefu wa fursa za ajira, wasi wasi kutokana na mashambulizi na misimamo mikali ya kidini. Lakini anapenda kukazia umuhimu wa wananchi kuchuchumilia misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano. Jimbo kuu la Mombasa linataka kuwekeza katika misingi ya elimu makini na endelevu ili kutoa fursa ya matumaini kwa vijana.

Lengo ni kuwajengea vijana uwezo wa kiuchumi, tayari kuchangia katika ustawi na maendeleo ya Kanisa na nchi ya Kenya katika ujumla wake. Wasikubali kutafuta mafanikio katika maisha kwa njia ya mkato, baraka kutoka kwa Mungu inakuja kwa njia ya matendo mema, matakatifu na adilifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.