2015-06-29 14:54:00

Naombeni sala zenu ninapoelekea Amerika ya Kusini: Equador, Bolivia na Paraguay


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Jumatatu, tarehe 29 Juni 2015, Sherehe ya Mitume Petro na Paulo, miamba wa imani, pamoja na kubariki Pallio Takatifu watakazovishwa Maaskofu wakuu na Mabalozi wa Vatican kwenye nchi husika, alitafakari na kusali kwa pamoja Sala ya Malaika wa Bwana pamoja na waamini na mahujaji waliokuwa wamemiminika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baba Mtakatifu anasema, Sherehe ya Mitume Petro na Paulo, inaadhimishwa sehemu mbali mbali za dunia, lakini kwa Roma, Sherehe hii inabeba uzito wa pekee kutokana na ushuhuda wa maisha uliofungwa kwa kuwamda damu yao ambayo imekuwa ni msingi wa Kanisa la Kristo. Hawa ni watu waliotoka mbali ili kuja kutangaza Habari Njema ya Wokovu, wakayasadaka maisha yao kwa ajili ya Injili ya Kristo iliyokuwa na kielelezo na dira ya maisha yao.

Baba Mtakatifu anasema, utukufu wa Mitume Petro na Paulo ni chemchemi ya furaha na ari kuu kwa waamini wa Roma, changamoto ya kuishi na kujitahidi kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo, hususan: imani na mapendo. Imani kwa yesu Kristo, Masiha na Mwana wa Mungu, ambaye Mtume Petro alimkiri na kumuungama, kabla ya kutoka kifua mbele kwenda kuwatangazia Watu wa Mataifa ukweli huu wa kiimani. Huu ni upendo ambao Kanisa linatumwa kuutekeleza kwa kuwwa na mwelekeo mpana wa kiulimwengu.

Katika Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko amemkumbuka Bikira Maria aliyekuwa ameambata na Mitume wa Yesu waliojenga Kanisa kwa damu yao. Petro Mtakatifu alimfahamu Bikira Maria Mama wa Mungu, akazama katika Fumbo la Maisha ya Kristo. Mtume Paulo akawatangazia Watu wa Mataifa utimilifu wa mpango wa kazi ya ukombozi kwa kuzaliwa Yesu Kristo wakati ulipotimia. Ni Mitume ambao walisaidia kueneza Ibada kwa Bikira Maria, Afya ya Warumi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mitume Petro na Paulo ni wenzi wa safari ya maisha ya kiroho inayomtafuta  Mwenyezi Mungu; ni viongozi wa hija ya imani na utakatifu wa maisha. Huu ni mwaliko wa kuwakimbilia katika maombi, ili waweze kuwasaidia waamini kuwa na mioyo wazi tayari kupokea ushauri wa Roho Mtakatifu pamoja na kukutana na jirani zao.

Baba Mtakatifu amewakumbusha kwamba, Ibada ya Misa Takatifu katika Sherehe ya Mitume Petro na Paulo, ameungana na Maaskofu wakuu walioteuliwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anawatakia heri na baraka ndugu na jamaa za Maaskofu hawa waliowasindikiza katika tukio hili ambalo kimsingi ni kielelezo cha umoja na mshikamano la Kiti cha Khalifa wa Mtakatifu Petro; kikolezo cha huduma ya ukarimu kwa wale waliokabidhiwa kwao na Mama Kanisa, ili waweze kutekeleza dhamana hii kwa ari na moyo mkuu. Uwepo wa ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox katika maadhimisho haya ni ushuhuda wa udugu uliopo kati ya Makanisa haya mawili.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, sala yake kwa siku hii ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya mji wa Roma: kiroho na kimwili; ili neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu iweze kuwalinda na kuwaongoza wananchi wote wanaoishi mjini Roma, ili waamini waweze kushuhudia utilimifu wa imani ya Kikristo kama walivyofanya Mitume Petro na Paulo, miamba wa imani.

Baba Mtakatifu amewashukuru wanasanii wa Roma na wawezeshaji wake, ambao katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo kadiri ya mapokeo, wanaonesha michezo mbali mbali na fedha itakayopatikana, itatumika katika utekelezaji wa miradi ya huduma ya upendo huko Nchi Takatifu na Mashariki ya kati.

Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaambia waamini na mahujaji waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwamba, kuanzia tarehe 5 hadi 13 Julai 2015 atakuwa na hija ya kitume nchini Equador, Bolivia na Paraguay, huko Amerika ya Kusini, eneo ambalo ni muhimu sana katika maisha yake. Anapenda kuonesha furaha yake ya dhati kabisa atakapokutana nao katika maeneo yao. Baba Mtakatifu anawaomba waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumsindikiza katika hija hii kwa njia ya sala na sadaka zao, huku akisindikizwa pia na maombezi na tunza la Bikira Maria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.