2015-06-29 15:42:00

Kweli kuna Wakristo waliosimama kidete kulinda, kutetea na kutangaza imani!


Bwana Severin Kalonga pamoja na familia yake kutoka Jimbo kuu la Dodoma, Tanzania ni kati ya umati mkubwa wa waamini na watu wenye mapenzi mema waliohudhuria Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumatatu tarehe 29 Juni 2015 kama sehemu ya maadhimisho ya Sherehe ya Mitume Petro na Paulo, miamba wa imani. Katika Ibada hii ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu Francisko amebariki Pallio Takatifu watakazovishwa Maaskofu wakuu majimboni mwao.

Ndugu Severin Kalonga katika mahojiano maalum na Radio Vatican anashukuru, anaomba ushirikiano na kuwataka Wakristo popote pale walipo kuiungama imani yao, kuhakikisha kwamba, wanaiadhimisha, wanaitekeleza na kuimwilisha katika maisha adili yanayojikita katika Amri za Mungu pamoja na kuishuhudia katika maisha ya sala na huduma.

Bwana Severin Kalonga kwa niaba ya familia yake anapenda kwanza kabisa kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kulipandisha adhi Jimbo la Dodoma na kuwa ni Jimbo kuu, kielelezo cha ukomavu wa imani. Hii ni changamoto kubwa kwa Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dodoma kushikamana na kushirikiana na Askofu mkuu Beatus Kinyaiya aliyekubali kupokea dhamana na wajibu wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifu watu wa Mungu Jimbo kuu la Dodoma kwa moyo mkuu na mnyofu.

Bwana Severin Kalonga na familia yake, wamepata nafasi ya kutembelea katika maeneo ya kihistoria yanayogusa undani wa imani ya Wakristo. Anasema, kweli kuna watu waliosimama kidete kulinda, kutetea na kuitangaza imani kwa Kristo na Kanisa lake kiasi hata cha kujisadaka maisha yao. Kuna watu walichezeshwa “Sindimba” kwenye Magofu ya Colosseo, wakapambanishwa na wanyama wakali, bila kukata tamaa, kwani walitambua kwamba, Yesu alikuwa pamoja nao! Hii ni changamoto kwa Wakristo kusimama kidete kulinda, kutetea, kutangaza na kuishuhudia imani inayomwilishwa katika matendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.