2015-06-29 08:07:00

Kwa mifano halisi; wafundisheni watu kusali, kuamini na kumshuhudia Kristo!


Wafundisheni watu kusali kwa kusali; watangazieni imani kwa kuamini na washuhudieni kwa njia ya matendo. Haya ndiyo mambo makuu matatu yaliyopewa kipaumbele cha kwanza katika mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Mitume Petro na Paulo, miamba wa imani, Jumatatu, tarehe 29 Juni 2015 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Katika Ibada hii, Baba Mtakatifu amebariki Pallio Takatifu 46 watakazovishwa Maaskofu wakuu kwenye Majimbo yao makuu na Mabalozi wa Vatican katika nchi husika. Kadiri ya mapokeo, Ibada hii pia imehudhuriwa na ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, uliongozwa na Askofu mkuu Ioannis Zizioulas Adamaris wa Jimbo kuu la Pergamo.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake anasema, Liturujia ya Neno la Mungu inaonesha mateso na madhulumu waliyokumbana nayo Wakristo wa Kanisa la mwanzo; mambo ambayo hata leo hii bado yanaendelea sehemu mbali mbali za dunia, na wakati mwingine, yakifumbiwa macho kana kwamba, hayapo! Baba Mtakatifu amekazia kwa namna ya pekee, kuhusu ujasiri ulioneshwa na kushuhudiwa na Mitume pamoja na Wakristo wa Kanisa la mwanzo.

Ni ujasiri uliowawezesha kusimama kidete hata wakathubutu kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji, licha ya kifo na madhulumu yaliyokuwa yanawaandama kila siku ya maisha yao. Mitume na Wakristo hawa ndio wanaoendelea kuheshimiwa hadi leo hii, changamoto kwa waamini kujikita katika sala, imani na ushuhuda!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Jumuiya ya kwanza ya Wakristo ilikuwa ni Kanisa linalosali, kama inavyojionesha kwenye Mapango mengi yaliyoko mjini Roma. Huko waamini hawakukimbilia kujificha kwa kuogopa madhulumu, bali yalikuwa ni maeneo ya sala, ili kuitakatifuza Siku ya Bwana na kumwabudu Mwenyezi Mungu ambaye kamwe hawezi kuwasahau watoto wake.

Jumuiya ya Mitume Petro na Paulo inawafundisha waamini kwamba, Kanisa linalosali ni Kanisa ambalo limesimama imara; Kanisa linalotembea na kwamba, Mkristo anayesali, Ukristo wake unalindwa, unahifadhiwa na kuenziwa kwa kutambua kwamba, Mkristo huyo hayuko peke yake. Mwenyezi Mungu daima anasikiliza sala za waja wake na kuwaokoa kwa njia ya Malaika wake watakatifu dhidi ya hatari, nguvu za kifo, mitego ya shetani, ili kuwaonesha njia na kuwawashia tena moto wa matumaini; ili aweze kuwafariji na kuwaganga mioyo yao iliyopondeka na kuvunjika ndani mwao.

Ni msaada unaowawezesha waamini kuamka kutoka katika ndoto ili kukumbatia mambo msingi katika maisha; kwa maneno mafupi, Mwenyezi Mungu anataka kuwahakikishia waja wake kwamba, hawako pweke! Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyoendelea kutenda hadi leo, kwa kuwapatia waamini Malaika mlinzi, ili wasishikwe na woga wala kushindwa kuamini; wasiwe na furaha kupita kiasi na kushindwa kumfungulia Kristo mlango wa maisha yao. Hakuna Jumuiya ya Kikristo inayoweza kusonga mbele pasi na sala inayowawezesha kukutana na Mwenyezi Mungu.

Ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu katika ahadi zake na kamwe hawezi kuwaacha watoto wake. Kwa njia ya sala, mwamini anaonesha imani na matumaini yake na hapo Mwenyezi Mungu anaonesha pia uwepo wake wa karibu, hata wakati mwingine kwa njia ya zawadi ya Malaika na wajumbe wake watakatifu.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, jambo la pili ni imani, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu kamwe hawezi kuwaondoa watoto wake ulimwenguni wala kuwaondolea mateso na magumu wanayokabiliana nayo, bali anawajalia nguvu ya kuweza kuyashinda yote. Ni mwamini wa kweli anayethubutu kusema, kwa hakika Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. Katika historia ya Kanisa daima kumekuwepo na nguvu kutoka ndani na nje, zinazotaka kuliangamiza Kanisa, lakini hadi leo hii bado linasonga mbele.

Lakini yote haya yamepita na Mwenyezi Mungu ndiye aliyebaki amesimama imara. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, zimepita falme, watu, tamaduni, mataifa, siasa na watu wenye nguvu, lakini Kanisa ambalo limesimikwa katika mwamba thabiti, ambao ni Yesu Kristo linaendelea kudumu, licha ya dhoruba na magumu yanayolikumba na kulitikisa kutokana na dhambi; lakini amana ya imani inabaki katika huduma, kwani Kanisa si la watu binafsi bali ni la Kristo, anayeliendeleza na kulilinda kwa njia ya utakatifu wa maisha na kwa mifano ya Mitume Petro na Paulo. Waamini kwa jina la Yesu Kristo wametenda miujiza, wakawapenda hata adui za ona kushuhudia imani yao thabiti.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, jambo la tatu ni ushuhuda unaomwilishwa katika matendo, kama inavyojionesha kwa njia ya Mitume Petro na Paulo, waliomwaga damu yao kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa; wakakinywea Kikombe cha Bwana, wakawa rafiki zake Mungu. Mkristo pasi na ushuhuda, huyo ni tasa; ni sawa na mti mkavu ambao hauwezi kuzaa matunda; ni sawa na kisima kilichokauka hakiwezi kutoa maji. Kanisa limeweza kushinda ubaya kwa njia ya ushuhuda makini na wa kweli uliotolewa na watoto wake kwa kutambua kwamba, Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu aliye hai.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha Maaskofu wakuu kwamba, Pallio Takatifu watakazovishwa Majimboni mwao, ni alama ya Kondoo anayebebwa na Yesu mabegani mwake, kielelezo cha dhamana ya kichungaji na changamoto ya kuwa kweli ni wachungaji wema. Ni alama ya umoja na mshikamano na Kiti cha Khalifa wa Mtakatifu Petro na waandamizi wake pamoja na Maaskofu wote.

Katika Ibada hii, Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu wakuu wakazie mambo makuu matatu; Sala, Imani na Ushuhuda. Watu wanataka kuona viongozi na mabingwa wa sala; wanaoweza kuwafundisha waamini wao jinsi yak usali vyema zaidi, kwa kuwakabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu anayewaokoa na vifungo vyote vinavyowakabili katika maisha. Mwenyezi Mungu kwa wakati uliokubalika, atamtuma Malaika wake kuwaokoa watu wake kutoka katika utumwa na malimwengu. Maaskofu wakuu wapya wawe ni Malaika na vyombo vya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kanisa linawahitaji watu na walimu wa imani, wanaothubutu kuwafundisha waamini wao kutokuwa na woga wa akina Herode, wanaoendelea kulitesa na kulinyanyasa Kanisa. Hakuna Herode mwenye nguvu ya kuweza kuzima mwanga wa matumaini, imani na upendo kwa mtu anayemwamini Yesu Kristo.

Kanisa linawahitaji mashuhuda wanaotangaza Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Hawa ni mashuhuda jasiri, wenye mvuto na mashiko; wasioona aibu kumshuhudia Kristo na Msalaba wake mbele ya wakuu wa ulimwengu huu. Ni watu wanaoendelea kufuata ushuhuda wa Mitume Petro na Paulo pamoja na mashuhuda wengi wa imani katika historia na maisha ya Kanisa. Hawa ni Wakristo wa madhehebu mbali mbali walioshiriki katika ujenzi na ukuaji wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu Francisko ametambua uwepo wa ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza, ulioshiriki katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo.

Ushuhuda wa kweli anasema Baba Mtakatifu Francisko katika kuhitimisha mahubiri yake, hauna kinzani na unaambata maisha, kwa njia ya maneno, lakini zaidi kwa matendo, kama namna ya kuwafundisha wengine. Maaskofu wakuu wawafundishe watu kusali kwa kusali; kutangaza imani kwa kuamini na kutoa ushuhuda kwa njia ya ushuhuda unaomwilishwa katika matendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.  








All the contents on this site are copyrighted ©.