2015-06-28 09:43:00

Mwanadamu ana dhamana ya kiutu na kimaadili kutunza vyema mazingira!


Waraka wa Kitume uliotolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” ni muhimu sana katika mchakato wa uzalishaji wa chakula na uhakika wa usalama wa chakula kutoka katika sekta ya kilimo. Juhudi hizi hazina budi kujikita katika kanuni maadili na haki ya chakula kwa wote.

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna kundi kubwa la watu linalokabiliwa na baa la njaa pamoja na utapiamlo wakutisha, changamoto endelevu kwa Jumuiya ya Kimataifa. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanayo dhamana kubwa ya kuhakikisha kwamba, haki ya chakula inapatikana kwa wote, hasa wakati huu Jumuiya ya Kimataifa inapoendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ikumbukwe kwamba, haki ya chakula ni kigezo muhimu katika mchakato wa uhakika wa usalama wa chakula duniani. Haya ni kati ya mambo msingi yaliyojadiliwa kwenye Kongamano la kimataifa kuhusu “imani, kilimo, chakula na mazingira” lilifanyika, kwenye Onesho la Chakula Kimataifa, Milan Expo 2015, kuanzia tarehe 26 hadi tarehe 29 Juni 2015. Kongamano hili limehudhuriwa pia na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Kardinali Turkson amegusia kuhusu changamoto zinazoendelea kuikabili Jumuiya ya Kimataifa kuhusiana na masuala ya uhakika wa usalama wa chakula na athari za mabadiliko ya tabianchi na jinsi ambavyo Jumuiya ya Kimataifa inavyoweza kuzivalia njuga changamoto hizi, kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume kuhusu utunzaji bora wa mazingira.

Kardinali Turkson anakiri kwamba, kula chakula ni tendo la kimaadili na kiutu, ndiyo maana chakula kinapaswa kuwa ni haki ya kila mtu pasi na ubaguzi na kwamba, hii ni changamoto kwa wote na wala si kwa ajili ya viongozi wa kisiasa peke yao. Viongozi wa kidini pia wanamchango wao katika mchakato unaopania kuhakikisha usalama wa chakula na utunzaji bora wa mazingira. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba: uzalishaji wa chakula na sekta ya kilimo vinakuambatiana barabara kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu, kwani hali ilivyo kwa sasa inaonesha msigano mkubwa kati ya mambo haya makuu mawili.

Kwa wengi, chakula kinaweza kupatikana kwenye maduka makubwa ya bidhaa, dhana inayotenganisha uzalishaji wa chakula kinachotumika pamoja na shughuli za ugavi na uchumi zinavyoweza kuathiri uelewa kuhusu chakula. Hatua hii ni kubwa na inafichika sana machoni pa wengi anasema Kardinali Turkson. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume kuhusiana na utunzaji bora wa mazingira anakaza kusema: kuna uhusiano wa dhati kati ya: mazingira, kilimo na chakula, mwaliko wa kutambua kwamba, mwanadamu ni sehemu muhimu sana katika ulinzi na utunzaji wa mazingira, kwani asili yake ni udongo “Adamah”.

Kardinali Turkson anasema, kuna haja ya kuwa na majibu muafaka kutoka kwa binadamu, ili kuweza kuwa na mfumo bora wa lishe, kwa kulinda na kutunza mazingira yanayomhifadhi na kumlisha mwanadamu. Hapa binadamu anapaswa kupewa msukumo wa pekee badala ya mwelekeo wa sasa unaotoa mwanya kwa nguvu ya soko na matokeo yake, watu wanatafuta faida kubwa na hiki ni chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira.

Mwanadamu akipewa kisogo na badala yake, faida ikapewa kipaumbele cha kwanza, hapo mwanadamu atakuwa anajichumia majanga na maafa kwa siku za usoni. Uharibifu mkubwa wa mazingira una athari kwa maisha, ustawi na maendeleo ya binadamu. Hapa ndiyo maana, Baba Mtakatifu Francisko  katika Waraka wake wa kitume juu ya utunzaji bora wa mazingira, anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuwa makini na maendeleo ya sayansi na teknolojia yanayotaka kumtawala na kumdumaza mwanadamu katika masuala ya kiuchumi na kisiasa badala ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.  

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.