2015-06-28 10:46:00

Mkataba na Palestina: Kanisa Katoliki halitafuti upendeleo wa pekee!


Hivi karibuni, Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, kwa niaba ya Vatican na Bwana Riad Al Malki, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Mamlaka ya Palestina, waliwekeana mkataba wa ushirikiano kati ya pande hizi mbili ambao umegawanyika katika vipengele 32 vinavyoundwa na sura nane.

Tamko la pamoja kati ya pande hizi mbili linaonesha sehemu muhimu za maisha na utume wa Kanisa nchini Palestina. Vatican inaunga mkono suluhu ya kudumu kati ya Palestina na Israeli, itakayowezesha kuwa na amani na maridhiano kati ya watu, tayari kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu. Mkataba huu utaanza kutekelezwa rasmi pale pande zote mbili zitakaokuwa zimeridhia.

Askofu mkuu Gallagher anasema kwamba, Mkataba kati ya Vatican na Mamlaka ya Palestina ni ni mwendelezo wa hatua kubwa ambayo imekwishafikiwa na Mamlaka ya Palestina, kiasi cha kutambuliwa na Umoja wa Mataifa katika kikao chake kilichofanyika kunako tarehe 29 Novemba 2012, kwa kuitambua Palestina kuwa ni mwanachama mtazamaji wa Umoja.

Mkataba huu unalenga pamoja na mambo mengine, kuimarisha uhusiano kati ya Vatican na Palestina. Ni matumaini ya Vatican kwamba, Palestina itaweza kuwa nchi huru inayojitegemea haraka iwezekanavyo. Mchakato wa misingi ya haki na amani, unaweza kuendelezwa ikiwa kama unajikita katika majadiliano ya moja kwa moja na pande zinazohusika kwa kuungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa, ili ziweze kufanya maamuzi magumu yatakayosaidia kupatikana kwa amani na utulivu katika Nchi Takatifu.

Askofu mkuu Gallagher anakaza kusema mkataba huu hautoi upendeleo wowote kwa Kanisa Katoliki huko Palestina, bali unatambua maisha na utume wa Kanisa nchini Palestina. Pande hizi mbili zimeonesha utashi wa kutaka kushirikiana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Palestina. Mkataba huu ni kielelezo makini cha majadiliano na ushirikiano kati ya waamini wa dini mbali mbali ili kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani, tofauti kabisa na hali inavyojitokeza huko Mashariki ya kati ambako bado Wakristo wananyanyaswa, wanadhulumiwa na kuuwawa kikatiliki kutokana na imani yao.

Waamini wa dini mbali mbali wanahamasishwa kujenga na kudumisha uhuru wa kuabudu na dhamiri nyofu, ili kweli Palestina iweze kuwa ni mfano bora wa kuuigwa huko Mashariki ya Kati, ambako kuna idadi kubwa ya waamini wa dini ya Kiislam. Vatican inapenda kuendelea kuimarisha mchakato wa haki, amani, upatanisho na maridhiano huko Mashariki ya kati. Mkataba unaihamasisha Palestina kujifunga kibwebwe kupambana na vitendo vya kigaidi huko Mashariki ya kati. Familia ya Mungu nchini Palestina, imepokea hatua hii kwa moyo wa shukrani na matumaini makubwa kwa siku za usoni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.