2015-06-28 15:28:00

Bila huruma ya Mungu, wewe ungekuwa kama soli ya kiatu!


Mpendwa Msikilizaji wa kipindi cha  Hazina Yetu, Tumsifu Yesu Kristo. Tunakusalimu kutoka Radio Vatican inayokuletea ujumbe wa huruma ya Mungu kama ulivyoandikwa na Baba Mtakatifu Francisko ndani ya Misericordiae vultus yaani uso wa huruma; kwa wakati huu tunapoelekea kuuzindua Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Daima na daima, Mungu wetu amejidhihirisha kwa watu wake kuwa ni Mungu mwenye huruma na msamaha. Daima anawasamehe wanaotubu makosa yao. Anatuhurumia nasi daima katika udhaifu wetu. Pasipo huruma ya Mungu, tungekuwaje? Kila mmoja anajifahamu alivyo katika uhalisia wa moyo wake. Wakati mwingine hata sisi wenyewe tunajitilia mashaka, tunakuwa na wasiwasi kutokana na matendo yetu tuyafanyayo sirini na hata hadharani pia.

Hali hiyo itusadikishe kwamba, sisi sote tunahitaji huruma ya Mungu. Mpendwa msikilizaji wa Kipindi hiki kilichojaa maneno ya huruma ya Mungu; sadiki kwamba, hakuna mtu ambaye anaishi pasipo kuhitaji huruma ya Mungu na ya binadamu wenzake. Mshairi mara mmoja aliwahi kuhoji; hivi inakuwaje hata jambazi ambaye anawatendea wenzake maovu, anaiba, anajeruhi na  hata kuua watu;  siku akikamatwa jambazi huyo na kuanza kuadabishwa, huwa analia na kusema ‘tafadhali sana jamani nioneeni huruma mwenzetu’!! Ajabu kweli! Wakati yeye hakuwa na huruma katika kuiba na kuwatendea wengine vibaya.

Mfano huo mdogo wa mshairi utukumbushe kwamba sisi sote tunahitaji huruma ya Mungu. Watu wote wema, kwa waovu tunahitaji huruma ya Mungu. Jinsi Mungu Bwana wetu anavyowaangazia jua lake waovu kwa wema, vivyo hivyo huwaelekezea uso wake mpole na wa huruma wema kwa wabaya. Sisi sote tu watoto wa Mungu na tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, na kwavyo tukashirikishwa hulka ya utakatifu wa Mungu inayojidhihirisha katika wema, upendo na huruma. 

Polepole katika maisha yetu, huwa tunajivua sisi wenyewe tunu hizo. Kila mmoja anashuhidia, hakuna hata mtoto mmoja anayezaliwa akiwa mkatiri, mkorofi  hana huruma. Watoto wote wanazaliwa wazuri, wanaopendeza na kuvutia kwa kila mtu hata kila mtu anatamani kumshika na kumtabasamulia mtoto. Na tabasamu la mtoto linavutia kwa sababu halina hila wala unafiki, sauti yake ni karimu, ni dhahiri haina chembe ya unafiki.

Polepole, katika maisha ya familia isiyo na huruma au jamii isiyojua upendo wala huruma, inayoshabikia maovu kama ndiyo falsafa ya maisha, ndimo mtoto anamojifunza ukorofi, ukatiri, uzandiki, kiburi, jeuri na kila aina ya ukurutu wa uovu. Aliyekuwa mwema na mkarimu, anaanza kuwa mkorofi, mchoyo, mwizi, mu-wivu mwenye kuwatakia wenzake mabaya. Bahati mbaya sana tabia hizo mtu huweza pia kujifunza hata Kanisani; na ndiyo maana Baba Mtakatifu analialika Kanisa, kurudi katika Misingi. Na misingi hiyo anaidhihirisha wazi kabisa; yaani upendo unaomwilishika katika huruma.

Anapolialika Kanisa zima kurudi katika misingi; hakuna yoyote anayeachwa nje. Binadamu wote turudie wema ule wa Mungu uliopandwa ndani mwetu kwa kuumbwa kwetu wanadamu. Sote tunaomsadiki Kristo, msingi wetu ndiyo upendo, wema na huruma ya Mungu, ambayo kwayo tumeumbwa, ili tumjue, tumpende, tumtumikie na tukaokoke milele. Tunapoisahau misingi haswa ya imani yetu, hapo ndipo tunapoanza kugeuza fikra zetu na ndoto zetu na tabia zetu kuwa ndio dira ya Kanisa; na ndipo haswa kwa kufanya hivyo tunakengeuka na kuchafua sura takatifu ya Mama Kanisa.

Kwa Mwangwi wa Mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko ndani ya Misericordiae vultus yaani uso wa huruma, tuifananishe na nini huruma ya Mungu? Huruma ya Mungu ni kama dira ya maisha na utume wa Kanisa. Huruma ya Mungu ni kama usukani unaonyoosha matairi ya gari takatifu (yaani Kanisa), yakanyage pazuri na safari iwe salama. Huruma ya Mungu ya Mungu ni kama maua yanayochanua daima na kuleta harufu nzuri ndani ya Kanisa na ulimwenguni kote.

Huruma ya Mungu ni Kama nuru inayotufanya tutembee vizuri kwa sababu inatung’arisha hata kama tu wachafu. Huruma ya Mungu ni kama sabuni inayotutakasa na madoa yote na vumbi la kuangukaanguka katika maisha yetu. Huruma ya Mungu ni kama mwavuli unaotukinga wakati wa mvua kali ya maisha yetu. Huruma ya Mungu ni kivuli kinachotukinga tusiungulie na jua kali la maisha yetu. Huruma ya Mungu ni kama taa ya kijani barabarani inayotupa ruhusa na kututia moyo twende, twende mbele zaidi. Huruma ya Mungu haswa, ndiyo inayotupatia ujasiri mkuu.

Hata kama kwa ndani tunajifahamu tulivyovunda na hata kuoza kabisa, lakini kwa huruma ya Mungu inayotulinda, inayotuhifadhi na kufunika aibu zetu, tunaendelea kutembea huku tumeinua vichwa. Sisi wanadamu huwa tuna tabia ya kujivua fahamu katika uovu wetu na kujisahaulisha hali ya udhambi wetu. Tunatenda kila dhambi tukidhani kuwa hakuna anayetuona! Ukweli ni kwamba, tunapotenda dhambi, hatuwaoni wale wanaotuona. Jirani zetu wanatuona kabisa, ila kwa msaada na huruma ya Mungu, wanatuhifadhi tu.

Tunafanya kila aina ya uhaini na watu wanakaa kimya tunadhani hawajui, na sie tunaendelea kujiamini katika madhambi yetu, na kuzidi kujilundikia vifusi vya dhambi! Ukweli ni kwamba, sio kwamba watu hawazijui dhambi zako, wanazijua sana, ila usione wanakaa kimya, hujui wanaziongea wakati gani. Na kama hawajaongea, bado hawajapata tu nafasi ya kukuchambua vizuri. Ni kwa nini?? Ni kwa sababu huruma ya Mungu inakufunika, kukulinda, kukuvumilia na kukusaidia. Katika yote hayo yote, kwa nini tusiishukuru huruma ya Mungu? Kwa nini tusiitangaze huruma ya Mungu? Kwa nini sisi wenyewe tusiwe na huruma kwa wenzetu? Ee Yesu mwenye moyo mpole na mnyenyekevu, ufanye mioyo yetu ifanane na Moyo wako.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni  mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.