2015-06-27 10:01:00

Amani na utulivu ni kichocheo cha maendeleo endelevu!


Askofu mkuu Martin Kuvuva Musonde wa Jimbo kuu la Mombasa, Kenya ni kati ya Maaskofu wakuu 46 wanaotarajiwa kupewa Pallio Takatifu wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni.

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, Mombasa ni mlango wa imani kwa Kanisa nchini Kenya. Ni eneo ambalo lina utajiri mkubwa wa vivutio kwa watalaii kutoka ndani na nje ya Kenya. Mombasa imebahatika kuwa na watu kutoka katika makabila, lugha, jamaa na dini mbali mbali, ambao wanachangamotishwa kuishi kwa amani, upendo na mshikamano wa kitaifa, kwa kutambua kwamba, tofauti zao ni utajiri mkubwa na kichocheo kikuu cha maendeleo.

Askofu mkuu Kivuva ana mshukuru Mwenyezi Mungu kwa mafanikio makubwa yaliyokwisha kupatikana Jimbo kuu la Mombasa katika ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu: kiroho na kimwili. Waamini wanaendeleo kushuhudia na kumwilisha imani yao katika matendo, licha ya changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo kila siku. Jimbo kuu la Mombasa lina Parokia 51 zinazohudumiwa na Wapadre 89 na kuna idadi kubwa ya watawa na majandokasisi wanaoendelea kunolewa katika maisha na utume wa Kipadre.

Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde anasema, Mombasa inakabiliwa na changamoto nyingi, na kati ya changamoto hizi ni kinzani za kidini zinazotokana na misimamo mikali ya kiimani; ulinzi na usalama; hofu na mashaka kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab.

Katika shida na mahangaiko haya yote, Askofu mkuu Musonde anaitaka Familia ya Mungu nchini Kenya, kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa. Amani na utulivu ni jina jipya la maendeleo endelevu ya binadamu. Kila mwananchi apanie kusimamia misingi ya haki na amani, ili waweze kufurahia maisha ma kudumisha maendeleo. Watambue kwamba, tofauti zao za kidini, kikabila na mahali anapotoka mtu ni utajiri na rasilimali kubwa kwa ajili ya maendeleo ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.