2015-06-26 16:00:00

Imarisheni misingi ya elimu na maadili; ndoa na utunzaji wa mazingira!


Chama cha Kimataifa cha Viongozi Wanawake Wakatoliki, kinaadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu kilipoanzishwa. Hiki ni chama ambacho kimekuwa na mchango wa pekee katika mchakato wa elimu na makuzi miongoni mwa wasichana, changamoto kwa vyama na wadau wengine kuiga mfano huu, ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo.

Elimu ni nyenzo muhimu sana inayowawezesha wasichana kuwajibika barabara; kwa kushuhudia imani na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake; furaha ambayo inamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Kwa njia hii, wasichana wanaweza kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa ulimwengu ulio bora zaidi kwa kujikita katika misingi ya Kiinjili.

Hii ni sehemu ya hotuba ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa, tarehe 26 Juni 2015 kwa Viongozi Wanawake Wakatoliki wanapoadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu Chama hiki kilipoanzishwa. Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu “Kuishi furaha ya Injili kama kiongozi”.

Hii ni changamoto ya kushuhudia katika maisha furaha ya kukutana na Yesu anayewaokoa na kuwaponya; kwa kukutana na Yesu, kuna wafanya waamini kuwa wazi kwa wengine, tayari kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu, hususan maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja na wale wanaoendelea kuogelea katika upweke. Haya ni Mapokeo kwa vyama vingi vya kitume ndani ya Kanisa ya kutaka kuwaonjesha wengine ukarimu na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Amana hii inapaswa kuendelezwa na kudumishwa.

Baba Mtakatifu anawakumbusha viongozi hawa wanawake kwamba, wanaowajibu wa kuhakikisha kwamba, wanawatangazia jirani zao Habari Njema juu ya Yesu anayewakirimia furaha na mwanga. Wao kama viongozi wanabahati ya kuweza kukutana na watu kutoka katika tamaduni na dini mbali mbali. Kumbe, hii inakuwa ni fursa ya kujenga na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuwaheshimu na kuwathamini wengine sanjari na kushuhudia imani na utambulisho wao wa Kikatoliki.

Baba Mtakatifu Francisko anasema katika Waraka wake wa kichungaji kuhusu utunzaji bora wa mazingira “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” anakaza kuhusu umuhimu wa malezi na majiundo ya utunzaji bora wa mazingira ili kiubadilisha mitindo na mawazo ya watu, ili hatimaye, kuweza kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo mintarafu uharibifu mkubwa wa mazingira, nyumba ya wote.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, viongozi hawa wataendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika utunzaji bora wa mazingira, kwa kupokea na kutunza wema na ubora ambao Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu katika ulimwengu huu. Tafakari hii ya kina inaweza kuwasaidia watu kuwa na amani na utulivu ndani mwao, kati yao na jirani zao pamoja na Mwenyezi Mungu. Huu ni mtindo mpya wa maisha mintarafu Injili; mambo yanayoweza kumwilishwa katika uhalisia wa maisha.

Baba Mtakatifu anasema, wanawake wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa; kwa kupewa nafasi wanayostahili ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake, mwaliko kwa wakuwaanda wasichana kuweza kutekeleza vyema dhamana na utume wao kwa siku za usoni, kadiri ya mapenzi ya Mungu. Wasichana waelimishwe kuhusu wito na mahusiano mema kati yao na wanaume; wawe tayari kushika nyadhifa mbali mbali ndani na nje ya Kanisa.

Katika maeneo ambayo bado kuna mfumo dume unaowanyanyasa na kuwadhalilisha wanawake na wasichana, chama hiki kinapaswa kujikita katika elimu na malezi bora. Wawasaidie wasichana wanaotaka kuwa watawa, waweze kutekeleza ndoto yao. Bikira Maria mfano wa umama wote kadiri ya Injili na moyo wa Mungu, awe kwao chemchemi, msaada na matumaini katika maisha na utume wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.