2015-06-19 16:36:00

Damu ya mashuhuda wa imani iwe ni mbegu ya umoja na chombo cha haki na amani


Neema na iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo. Hija ya kichungaji inayofanywa na Mheshimiwa sana Moran Mor Ignatius Aphrem wa pili wa Kanisa la Kiorthodox la Siro la Antiokia na Mashariki yote nalenga kuimarisha na kudumisha urafiki na udugu kati ya Makanisa ya Roma na Antiokia. Umoja ni kati ya mambo makuu yaliyopewa kipaumbele cha kwanza na Mtakatifu Ignatius wa Antiokia, ili Wakristo wote waweze kuunganika kiakili, katika sala, matumaini na mapendo; ili kwa pamoja waweze kuizunguka Altare ya Kristo inayowaelekeza kwa Baba yake wa mbinguni.

Hizi ni salam ambazo zimetolewa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana, akazungumza na kusali na Patriaki Moran Mor Ignatius Aphrem wa pili wa Kanisa la Kiorthodox la Siro la Antiokia na Mashariki yote ambaye anahitimisha hija yake hapa mjini Vatican, Ijumaa, tarehe 19 Juni 2015. Kunako mwaka 1971 Patriaki Mor Ignatius Jacob III alikutana na kuzungumza na Papa Paulo VI, waliohimiza umuhimu wa kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kuwa na umoja kamili unaoonekana kati ya Wakristo wa Makanisa haya mawili.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ilikuwa ni fursa ya kusali na kuungama Imani katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na hatimaye, kutoa tamko la pamoja, kama sehemu ya utekelezaji wa amri ya Kristo, ili wote wawe wamoja. Patriaki Mor Ignatius Zakka Iwas na Mtakatifu Yohane Paulo II walipiga hatua kubwa kwa kuweka mikakati ya kichungaji ambayo ingetekelezwa na waamini wa Makanisa haya mawili kwa ajili ya mafao ya wote.

Baba Mtakatifu anasema, kuna mambo mengi yamebadilika, lakini Kanisa limeendelea kuwa ni Kanisa la mashuhuda tangu mwanzo hadi nyakati hizi. Hadi leo hii kuna Wakristo wanaolazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na vita, nyanyaso na dhuluma wanazotendewa, kiasi cha kudhani kwamba, viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa hawana tena nguvu ya kuweza kupata suluhu ya kudumu kutokana na majanga yanayowakabili wananchi huko Mashariki ya Kati.

Baba Mtakatifu amemwalika Patriaki Moran Mor Ignatius Aphrem wa pili kusali kwa ajili ya kuwaombea watu wanaoendelea kuteseka kutokana na vita sehemu mbali mbali za dunia pamoja na kuwakumbuka Askofu mkuu Mor Gregorios Ibrahim na Askofu mkuu Paul Yazigi wa Kanisa la Kigiriki la Kiorthodox ambao walitekwa nyara, sasa yapata miaka miwili, lakini hawajulikani mahali walipo!

Wamewakumbuka Mapadre pamoja na waamini ambao wametekwa nyara na hatima yao hadi sasa haijulikani ili Bwana aweze kuwajalia neema na nguvu ya kuwa kweli ni vyombo vya msamaha, wahudumu wa upatanisho na amani. Damu ya mashuhuda wa imani iwe ni mbegu ya umoja wa Kanisa na chombo cha ujenzi wa ufalme wa Mungu unaojikita katika: haki na amani. Huu ni wakati wa kuimarisha urafiki na udugu kati ya Makanisa, ili kwamba, siku moja waweze kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa wakiwa wameungana, tayari kubadilishana amana na Mapokeo ya Makanisa haya mawili, kwa kutambua kwamba, kuna mambo mengi yanayowaunganisha kwa pamoja, kuliko yale yanayowagawa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.