2015-06-17 08:55:00

Lebanon ni mfano katika kukuza na kudumisha: haki, amani na maridhiano!


Upungufu wa Wakristo na pengine hatimaye kutoweka kwa uwepo wa Wakristo huko Mashariki ya Kati kuna madhara makubwa si tu kwa Kanisa bali hata katika eneo zima la Mashariki ya Kati. Ni maneno ya Kardinali Dominique Mamberti, Mwenyekiti wa Mahakama kuu ya Kitume ya Kanisa baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi nchini Lebanon kwa mwaliko wa Kardinali Bèchara Boutros Rai.

Hii ilikuwa ni nafasi ya kumshukuru Mungu kwa kuteuliwa kwake kuwa Kardinali na Mwenyekiti wa Mahakama kuu ya Kitume ya Kanisa; matukio ambayo yamekwenda sanjari na kufungwa kwa Mwezi wa Maria kwenye Madhabahu ya Bikira Maria Mama Yetu wa Lebanon. Kardinali Mamberti anasema, amebahatika kukutana na kuzungumza na viongozi wa Mahakama za Kikanisa na hivyo kubadilishana mawazo kuhusu utume na changamoto wanazokabiliana nazo kwa wakati huu.

Kardinali amekutana pia na Baraza la Maaskofu Katoliki Lebanon waliopembua kwa kina na mapana hali halisi ya Wakristo huko Mashariki ya Kati na changamoto zilizopo kwa sasa. Ilikuwa ni nafasi kwa Kardinali Mamberti kuwasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa Familia ya Mungu nchini Lebanon, hasa katika kipindi hiki kigumu cha historia na utume wa Kanisa huko Mashariki ya Kati.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufuatilia kwa karibu zaidi, matukio mbali mbali yanayojitokeza huko Mashariki ya Kati, kiasi cha kutishia amani, usalama, ustawi na mafungamano wa kijamii pamoja na maridhiano kati ya watu. Inasikitisha kuona kwamba, kwa takribani mwaka mmoja, wananchi wa Lebanon wameshindwa kufanya uchaguzi mkuu ili kumpata kiongozi atakayeongoza nchi kutokana na kinzani zinazoendelea kusikika sehemu mbali mbali za Lebanon.

Kardinali Mamberti anasema kwamba, amezungumza kwa kina na mapana na viongozi wa Kanisa huko Beirut pamoja na kukutana na viongozi wa Serikali na Bunge pamoja na wanasiasa. Amebahatika kufanya mkutano wa kiekumene na kidini na viongozi wakuu wa kidini huko Mashariki ya Kati, jambo linaloonesha kwamba, kuna uwezekano mkubwa kwa watu kuishi kwa amani na utulivu, licha ya tofauti zao za kidini na kiimani, daima wakitafuta mafao, ustawi na maendeleo ya wengi.

Kutokana na ukweli huu, Mtakatifu Yohane Paulo II alipenda kusema daima kwamba, Lebanon ni ujumbe makini kwa watu wa nyakati hizi katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano anasema Kardinali Mamberti. Hali ya Wakristo huko Lebanon inatisha sana kutokana na ukweli kwamba, wengi wao wanalazimika kuikimbia nchi ili kusalimisha maisha yao. Hali hii pia inawakumba waamini wa dini ya Kiislam kwa kutambua kwamba, vita haina macho!

Kardinali Mamberti anakiri kwamba, lakini waathirika wakuu ni Wakristo ambao wanashiriki kwa namna ya pekee katika shughuli mbali mbali za kijamii, kisiasa na kiuchumi nchini Lebanon, kwani hapa idadi ya Wakristo ni kubwa ikilinganishwa na waamini wa dini nyingine.

Kupungua na hatimaye kutoweka kwa Wakristo huko Mashariki ya Kati anasema Kardinali Mamberti litakuwa ni pigo kubwa huko Mashariki ya Kati kwani Wakristo nchini Lebanon wamekuwa mstari wa mbele katika kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene; katika ustawi na maendeleo ya nchi; kwa kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Wakristo wamekuwa wakitafuta mafao ya wengi na kamwe hawakutaka kupewa upendeleo wa pekee, hali ambayo imedumisha amani na utulivu. Kanisa la kiulimwengu linawashukuru na kuwapongeza Wakristo huko Mashariki ya Kati, na linaendelea kuwatia moyo ili waweze kusonga mbele kwa imani na matumaini, licha ya magumu na changamoto wanazokabiliana nazo kwa wakati huu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.