2015-06-17 09:59:00

Chuchumilieni utakatifu kama chachu ya Uinjilishaji mpya!


Wafuasi wa Kristo wanaaitwa kila siku ya maisha yao kuhakikisha kwamba, wanachukua Msalaba na kumfuasa Yesu Kristo aliye njia, ukweli na uzima. Hili ndilo jibu muafaka linalobubujika kutoka kwa mfuasi wa Kristo anayekubali na kuitikia kufuasa wito maalum wa kuwa mhudumu wa Mafumbo ya Kanisa.

Kutokana na dhamana pamoja na utume huu, wakleri kwa namna ya pekee wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanachuchumilia utakatifu wa maisha kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda makini, wenye mvuto na mashiko! Hii ndiyo changamoto endelevu, iliyotolewa na Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, alipokuwa anahitimisha mafungo ya wakleri kimataifa, yaliyokuwa yanafanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, hapa mjini Roma, kuanzia tarehe 10 hadi tarehe 14 Juni 2015.

Itakumbukwa kwamba, haya yalikuwa ni mafungo ya tatu kimataifa kuandaliwa na Chama cha Uamsho wa Kikristo kimataifa kwa kushirikiana na Chama cha Udugu wa Kikatoliki. Kardinali Stella ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Jumamosi jioni tarehe 13 Juni 2015, siku ambayo Wakleri walikuwa wanatafakari kuhusu umuhimu wa kuimarishwa na Roho Mtakatifu, ili waweze kuwa wafuasi na wamissionari mahiri, tayari kutoka kifua mbele kuwatangazia Watu wa Mataifa, Injili ya Furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Kardinali Stella amekazia umuhimu wa kuambata utakatifu wa maisha kama kikolezo cha Uinjilishaji mpya, dhamana inayoendelea kuvaliwa njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Kanisa ni taasisi ambayo kimsingi, mafanikio yake yanategemea kwa kiasi kikubwa utakatifu wa maisha wa watoto wake na wala si taaluma na weledi katika kutekeleza sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, ingawa ni muhimu pia.

Wakleri wahakikishe kwamba, kwa njia ya mfano wa ushuhuda wa maisha ambao ni sehemu ya mchakato wa utangazaji wa Injili ya Kristo, wanaweza kuwafikia watu wengi zaidi, kwa kuwavuta kukutana na kumwambata Yesu katika hija ya maisha yao ya kila siku. Bila mvuto wenye mashiko, Kanisa linaweza kuonekana kana kwamba, ni taasisi kama taasisi nyinginezo zinazotoa huduma kwa watu. Wakleri si watu huru wanaoweza kufanya wanavyopenda! La hasha!

Ni watu walioitwa, kumbe wanapaswa kupokea wito huu kwa unyenyekevu na moyo mkuu, ili Roho Mtakatifu aweze kuwaletea mageuzi katika maisha yao, tayari kujisadaka kwa ajili ya kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Furaha. Wakleri watambue na kuthamini uwepo endelevu wa Roho Mtakatifu katika maisha na utume wao. Utakatifu uwe ni chachu na kikolezo cha mchakato wa Uinjilishaji mpya.

Kwa upande wake, Padre Raniero Cantalamessa, mhubiri wa nyumba ya kipapa wakati wa tafakari yake, amekazia umuhimu wa Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Wakleri ambao ni wahudumu wakuu wa Mafumbo ya Kanisa. Anasema, wakleri ambao wako karibu sana na Chama cha Uamsho wa Kikristo, watambue na kuthamini nafasi ya Roho Mtakatifu katika maisha yao, kwani wamepakwa mafuta na kuimarishwa na karama za Roho Mtakatifu anayewasindikiza katika hija ya maisha na utume wao.

Kwa kupakwa mafuta, wamepewa pia karama na mapaji ya Roho Mtakatifu, anayewaongoza na kuwafunda ili kweli waweze kuwa ni vyombo vya Uinjilishaji vinavyojikita katika unyenyekevu, amani na utulivu. Wakleri watambue kwamba, wamepewa karama ya nguvu, uongozi na madaraka kwa ajili ya kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza Watu wa Mungu katika hija ya maisha yao ya kila siku.

Padre Raniero Cantalamessa anawakumbusha Wakleri kwamba, tayari walikwishakupokea Mapaji ya Roho Mtakatifu katika Sakramenti nyingine za Kanisa yaani: Ubatizo na Kipaimara. Mapaji na karama za Roho Mtakatifu zinaweza kudumaa na kushindwa kuzaa matunda yanayokusudiwa, ikiwa kama hazitaweza kutumiwa vyema kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo.

Wakleri wawe ni mfano wa manukato mazuri, yanayoacha harufu nzuri kila mara watu wanapokutana nao, kwa kushinda kiburi na majivuno; kwa kuganga na kuponya mapungufu ya kibinadamu ili kumpatia Yesu Kristo kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wao.

Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma, katika mahubiri yake wakati wa kufunga rasmi mafungo ya Wakleri kimataifa, kwenye Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Jumapili tarehe 14 Juni 2015, amewataka Wakleri kujenga na kudumisha utamaduni wa kusali, kutafakari Neno la Mungu pamoja na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa moyo wa uchaji na ibada. Wajenge ndani mwao utamaduni wa ukimya, ili kukutana na kuteta na Yesu katika hija ya maisha yao ya kila siku.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.