2015-06-09 10:52:00

Waamini wanachangamotishwa kuchuchumilia utakatifu wa maisha!


Mwaliko wa kuchuchumilia utakatifu wa maisha kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya, ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya mafungo ya tatu ya kiroho yatakayofanyika mjini Roma kuanzia 10 hadi tarehe 14 Juni 2015. Mafungo haya yatafanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano mjini Roma. Ni mafungo kwa ajili ya Wakleri, hasa wakati huu Mama Kanisa anapojielekeza zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, anawachangamotisha watoto wake, kushuhudia utakatifu wa maisha, kielelezo cha imani tendaji.

Mafungo haya ya kimataifa yameandaliwa na Chama cha Kitume cha Uhamsho wa Kikristo Kimataifa kwa kushirikiana na Chama cha udugu wa Kikatoliki, ili kuweza kuchochea karama ya Mungu iliyomo ndani mwao, kwa vile wamewekewa mikono na kupewa nguvu ya Roho wa upendo na moyo wa kiasi, ili kuweza kushuhudia ukuu wa Mungu katika maisha yao. Hawa ni watu ambao wanaitwa, wanageuzwa na kuimarishwa tayari kutumwa kushuhudia na kutagaza Injili ya Furaha kati ya watu wa Mataifa.

Hizi ni mada zitakazochambuliwa kwa kina na mapana wakati wa maadhimisho ya mafungo haya ya kimataifa yanayowashirikisha wajumbe 900; kati yao kuna Makardinali, Maaskofu, Mapadre na Mashemasi kutoka katika nchi 90. Taarifa zinazoonesha kwamba, Bara la Afrika katika mafungo haya linawakilishwa na wakleri 166 kutoka katika nchi 22.

Mafungo haya yatafunguliwa rasmi tarehe 10 Juni 2015 kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Kardinali Stanislaw Rylko, Rais wa Baraza la Kipapa la Walei. Kati ya wahamasishaji watakaotoa tafakari elekezi ni pamoja na Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa nyumba ya kipapa atakayejikita zaidi katika mada “tunaitwa kukumbatia utakatifu wa maisha kwa ajili ya Uinjilishaji mpya”. Tarehe 11 Juni 2015, Kardinali Peter Turkson ataongoza tafakari inayohusu upatanisho na Mungu. Siku hii wajumbe pia watapata nafasi ya kujipatanisha na Mungu kwa njia ya Sakramenti ya kitubio, ili kuonja gharama ya upatanisho na Mungu inayojikita katika huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Tarehe 12 Juni 2015, Siku kuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, siku maalum iliyotengwa kwa ajili ya kuombea Utakatifu wa Mapadre; jioni, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kutoa tafakari ya kina inayowaonesha kwamba, wamegeuzwa kwa njia ya upendo kwa ajili ya upendo. Atazungumza na Mapadre na hatimaye, kuadhimisha Fumbo la Ekaristi takatifu. Washiriki watapewa dhamana ya kuendeleza kazi ya kimissionari.

Tarehe 13 Juni 2015, Padre Raniero Cantalamessa atafanya tafakari ya kina kuhusu “Kuimarishwa ili waweze kuwa kweli ni mitume na wamissionari. Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri ataongoza Ibada ya Misa Takatifu. Baadaye jioni tafakari zitaendelea kama kawaida. Mafungo haya yatafungwa rasmi na Jumapili tarehe 14 Juni 2015 na Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.