2015-06-04 07:59:00

Yatakayojiri wakati wa hija ya kitume ya Papa Francisko mjini Sarayevo!


Haki, amani na upatanisho ni mambo msingi ambayo yatapewa kipaumbele cha kwanza na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Bosnia- Erzegovina. Hii itakuwa ni nchi ya kumi na nne kutembelewa na Baba Mtakatifu Francisko tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Hii ni safari ya nane ya kimataifa itakayofanywa na Baba Mtakatifu, Jumamosi tarehe 6 Juni 2015. Kardinali Vinko Puljic ndiye aliyemwalika Baba Mtakatifu Francisko kutembelea nchini Bosnia-Erzegovina.

Haya yamebanishwa na Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican hivi karibuni alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari mjini Vatican. Ratiba ya siku moja, katika kipindi cha masaa kumi na mawili, imesheheni mambo msingi ambayo Baba Mtakatifu anatarajiwa kuyatekeleza wakati wa hija yake ya kitume. Baada ya kutembelea Albania, kati ya nchi zilizoko pembezoni mwa Bara la Ulaya, Baba Mtakatifu kwa sasa anatarajiwa kutembelea Bosnia-Erzegovina nchi ambayo mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene unaendelea kupamba moto, ili kujenga amani, upendo, mshikamano na maridhiano kati ya watu.

Katika hija hii, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuandamana na Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini pamoja na Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa linalohamasisha umoja wa Wakristo. Matukio makuu mawili muhimu sana wakati wa hija ya Baba Mtakatifu. Mosi, ni adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu litakaloadhimishwa asubuhi katika Uwanja wa Michezo wa Kosevo.

Hapa ni mahali ambapo Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1997 aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, wakati ambapo vita ilikuwa imepamba moto. Papa Yohane Paulo II akawataka wananchi waanze mchakato wa kusameheana na kuombana msamaha, tayari kuanza ukurasa mpya wa maisha. Padre Lombardi anasema kwamba, katika adhimisho hili, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kukazia mambo makuu mawili: haki na amani; changamoto kubwa kwa wananchi wa Bara la Ulaya.

Tukio la pili ambalo linapewa kipaumbele cha  pekee katika hija hii ni wakati wa jioni, ambapo Baba Mtakatifu Francisko atakaposhiriki mkutano wa vijana wa kiekumene na kidini kwenye Kituo cha Vijana Kimataifa. Wawakilishi wa vijana kutoka katika dini mbali mbali watakutana na Baba Mtakatifu, tayari kujikita katika mchakato wa ujenzi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu bila kutawaliwa na kinzani za kikabila, kidini na kisiasa.

Padre Lombardi anasema, Baba Mtakatifu Francisko atakutana na kuzungumza na viongozi wa kisiasa na kidini karibu na Uwanja wa Ndege, kwenye Ikulu. Baba Mtakatifu atashirikisha mawazo na Baraza la Maaskofu Katoliki Bosnia-Erzegovina wakati wa chakula cha mchana kwenye Ubalozi wa Vatican. Baba Mtakatifu jioni anatarajiwa pia kukutana na kuzungumza na Wakleri pamoja na Watawa, Kwenye Kanisa kuu na baadaye atakutana pia na vijana wa Sarayevo kwenye Kituo cha Vijana kilichoanzishwa kwa heshima ya Mtakatifu Yohane Paulo II.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.