2015-05-26 08:19:00

Jubilei ya miaka 500 tangu alipozaliwa Mt. Filippo Neri, Mtume wa Roma


Mama Kanisa anadhimisha Jubilei ya Karne tano tangu alipozaliwa Mtakatifu Filippo Neri (1515- 2015). Tukio hili muhimu kwa maisha na utume wa Kanisa litafungwa rasmi hapo tarehe 26 Mei 2016. Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua na kuthamini mchango wa Mtakatifu Filippo  aliyezaliwa Jimbo kuu la Firenze, Italia tarehe 21 Julai 1515, akautumia muda wake mwingi kwa ajili ya utume kwa Mji wa Roma, kiasi cha kupatiwa jina la “Mtume wa Roma” amewaandikia ujumbe mahususi watawa wa Shirika la Mtakatifu Filippo Neri kwa kuwapongeza na kuwatia shime.

Mtakatifu Filippo Neri ni Padre aliyeyakita maisha yake kwa kujenga mahusiano ya karibu na Yesu Kristo, akajitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia watu waliokuwa wamekabidhiwa wake katika safari yao ya maisha ya kiroho. Ni muasisi wa vituo vya michezo vinavyoongozwa na kuratibiwa na Mama Kanisa. Vituo hivi vilikuwa ni chemchemi ya sala, tafakari ya Neno la Mungu, mahali pa kusikiliza na kusikilizwa; mahali muafaka pa kujiandaa kwa ajili ya kupokea Sakramenti za Kanisa na majiundo makini kwa maisha ya Kikristo. Hii ilikuwa ni huduma ya upendo kwa maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kwamba, kutokana na utume wa Mtakatifu Filippo Neri, Kanisa likatoa kipaumbele cha pekee kwa ajili ya wokovu wa roho za watu, kwa kuwasaidia na kuwaongoza katika hija ya imani. Mtakatifu Filippo akawa ni kiongozi wa waamini wengi waliojitosa kimasomaso kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo na wengine wakakumbatia maisha na utume wa Kipadre wakawa ni wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa.

Mtakatifu Filippo Neri alitoa kipaumbele cha kwanza kwa Sakramenti ya Upatanisho, akajitahidi kukaa katika kiti cha upendo na huruma ya Mungu hadi jioni kabisa, lengo lilikuwa ni kuwasaidia waamini wake kufanya hija katika maisha ya Kikristo kwa kuwa na matumaini. Ni kiongozi aliyebahatika kuwa na karama nyingi, mtu wa watu, mwenye furaha, mpole na mkarimu; mambo ambayo yalipata chimbuko lake kutokana na umoja na mshikamano ambao aliouonesha na kuujenga na Kristo Yesu kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Mtakatifu Filippo Neri alipenda kuwafundisha watu kusali kwa pamoja kama Jumuiya, akaonesha kwa mifano ya maisha yake maana ya kutubu na kufunga kama kielelezo cha furaha na amani ya ndani. Alikuwa ni mhubiri mahiri wa Neno la Mungu, aliyewaamini na kuwathamini watu, akawapatia nafasi ya kukua na kukomaa katika fadhila za Kikristo. Ni kielelezo makini cha utume endelevu wa Kanisa linalotumwa kushuhudia kwa wote upendo na huruma ya Mungu; mfano wa kuigwa katika maisha na utume wake wa Kipadre.

Baba Mtakatifu Francisko katika kumbu kumbu ya miaka mia tano tangu alipozaliwa Mtakatifu Filippo Neri anaendelea kubainisha kwamba, alikuwa ni mtu aliyependa kuishi katika ukweli na uhalisia wa mambo, akawafundisha watu umuhimu wa kumwilisha fadhila za Kikristo, nidhamu na dhamana ya kumpokea Yesu Kristo katika uhalisia wa maisha ya mtu. Alitambua kwamba, hija ya utakatifu wa maisha inajikita katika neema ya kubahatika kukutana na Yesu pamoja na watu wengine na kuwapokea kwa moyo wa ukarimu na mapendo.

Baba Mtakatifu anawataka Watawa wa Shirika la Mtakatifu Filippo Neri kujifunza kutoka katika shule ya mwanzilishi wao, kwa kuwa ni watu wa sala na mashuhuda wanaowavuta wengine kwa Kristo. Vijana wa kizazi kipya wanahitaji kuona ushuhuda wa watu wanaosali na wanaofahamu kuwafundisha kusali vyema. Ni Mtakatifu aliyekuwa na Ibada ya pekee kwa Fumbo la Ekaristi Takatifu linalopaswa kuadhimishwa, kubudiwa na kumwilishwa katika maisha, kwani ni chemchemi inayobubujikia katika roho za watu.

Kwa njia hii, Yesu Kristo anakuwa kweli ni chemchemi ya furaha na matumaini kwa waja wake. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaweka watawa na walei wote wa Shirika la Mtakatifu Filippo Neri chini ya ulinzi na tunza ya Maria, Bikira na Mama.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.