2015-05-25 11:23:00

Wakristo 170 waimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara wakati wa Pentekoste


Siku kuu ya Pentekoste, Kanisa linaadhimisha siku ya kuzaliwa kwake, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, akawajaza nguvu na mapaji tayari kwenda kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia kwa njia ya maneno, lakini hasa zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha ya Kikristo. Siku kuu ya Pentekoste, ni siku maalum ya waamini walei wanaohamasishwa na Mama Kanisa kujikita katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu sanjari na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Padre Chesco Msaga, Makamu Askofu, Jimbo kuu la Dodoma, katika mahubiri yake kwa maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba ameikumbusha Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dodoma kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanashiriki katika ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo, hivyo wanatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko.

Roho Mtakatifu anawakirimia waamini mapaji wanayopaswa kuyafanyia kazi kwa ajili ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa pamoja na kushiriki katika ustawi na maendeleo ya jirani zao. Waamini wawe ni Askari makini wa kulinda, kutetea na kudumisha: imani, maadili na utu wema. Wawe na ujasiri wa kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa kwa kukataa kutumbukizwa katika masuala yanayohatarisha amani na mafungamano ya kijamii.

Padre Chesco anawataka waamini wajitahidi kukimbilia upendo na huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho kwani utume huu Yesu Kristo amelikabidhi Kanisa ambalo ni Sakramenti ya wokovu. Waamini wanaweza kuwa na amani na utulivu wa ndani kwa njia ya huduma kwa jamii, lakini zaidi wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wawe ni vyombo na watetezi wa ukweli, haki na amani katika jamii.

Mapaji waliyokirimiwa na Roho Mtakatifu yawawezeshe kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu kwa kujikita katika kudumisha haki jamii, utu na mafao ya wengi. Katika Siku kuu ya Pentekoste, waamini 170 wameimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara. Hawa ni wale ambao wanatoka katika vigango vya: Kanisa kuu, Ntyuka, Ng’ong’ona, Mzuwe na Michese.

Na Rodrick Minja.

Dodoma, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.