2015-05-25 10:19:00

Baa la umaskini bado ni tishio kubwa kwa ustawi na maendeleo ya wengi!


Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa anapongeza juhudi zinazofanywa na Umoja wa Mataifa kwa kushirikisha serikali mbali mbali katika majadiliano ili kupembua kwa kina na mapana mapungufu yaliyojitokeza katika utekelezaji wa Malengo ya Mendeleo ya Millenia yaliyokuwa yamebainishwa na Jumuiya ya Kimataifa hadi kufikia mwaka 2015. Majadiliano haya ni muhimu katika kuibua na kupanga mikakati ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo baada ya mwaka 2015. Lengo ni kupambana na umaskini ili kupata maendeleo endelevu.

Ujumbe wa Vatican kwenye mkutano huu uliofanyika hapo tarehe 19 Mei 2015 umekazia pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inatekeleza ahadi zake na kupima matokeo yaliyofikiwa. Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ndio wanaopaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika majadiliano ya kimataifa.

Ufuatiliaji makini ni muhimu sana kwa Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa maendeleo endelevu pamoja na kuzingatia tathmini zinazofanywa katika nchi husika katika kuangalia mafaniko na mapungufu yaliyojitokeza katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia. Tathmini hii ifanyike pasi na shuruti kwa kuhamasisha nchi husika kutekeleza dhamana hii kwa ajili ya mafao ya watu wake. Mwelekeo uwe ni kwa ajili ya kujenga na wala si kuhukumu na kubainisha maeneo ambayo yanapaswa kufanyiwa maboresho zaidi.

Askofu mkuu Auza anasema, matokeo yatakayopatikana kutoka katika nchi mbali mbali, yafikishwe kwenye Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya ufuatiliaji mpana zaidi, ili kuziba mapengo ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia. Jumuiya ya Kimataifa, haina budi kuzisaidia Nchi zinazoendelea ili kutekeleza kazi hii kwa ufanisi kwa kuziunga mkono na kuzipatia mwongozo; lengo ni maendeleo endelevu ya binadamu, lakini zaidi maskini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.