2015-05-24 08:45:00

Askofu mkuu Oscar Romero: Baba wa maskini, mtetezi wa wanyonge na umoja


Mwenyeheri Oscar Romero alikuwa kweli ni mtu wa Mungu, mtu wa Kanisa, Baba na mtetezi wa maskini na wanyonge; shuhuda wa amani, umoja na upatanisho unaojikita katika uhalisia wa maisha. Hivi ndivyo Baraza la Maaskofu Katoliki El Salvador linavyompamba Mwenyeheri Oscar Romero katika barua yao kwa Familia ya Mungu nchini El Salvador wakati wa kumtangaza kuwa Mwenyeheri, hapo tarehe 23 Mei 2015.

Maaskofu wanakumbusha kwamba, mara tu alipouwawa kikatili Askofu mkuu Oscar Romero wa Jimbo kuu la San Salvador, macho ya walimwengu yalielekezwa nchini humo ili kuonesha mshikamano wa umoja na upendo, kati yao ni ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, ambaye baada ya miaka mitatu, kunako tarehe 6 Machi 1983 alitembelea San Salvador na kusali kwenye kaburi la Askofu mkuu Oscar Romero.

Baraza la Maaskofu Katoliki El Salvador linasikitika kusema kwamba, mchakato wa kumtangaza Oscar Romero kuwa Mwenyeheri, ulichafuliwa na baadhi ya watu ambao “walimchafulia” jina kwa kutumia utambulisho na karama zake. Kauli mbiu aliyoiandika kwenye Nembo yake ya Kiaskofu  ni “Kujisikia pamoja na Kanisa”, dhana inayojikita katika umoja na mshikamano wa Kikanisa. Umoja wa Kanisa ni kati ya tema ambazo zilipewa kipaumbele cha pekee katika barua za kichungaji za Mwenyeheri Oscar Romero.

Kanisa lipo kwa sababu linatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia sanjari na maadhimisho ya Fumbo la Pasaka. Askofu mkuu Osca Romero alitaka kujenga Kanisa la El Salvador mintarafu changamoto zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na kufafanuliwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Amerika ya Kusini katika mkutano wao maarufu wa Medellìn.

Dhana ya umaskini kadiri ya tafakari ya Mwenyeheri Oscar Romero ilikuwa inabubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu na wala si katika masuala ya kisiasa na kwamba, upendeleo kwa maskini ni utume ambao ulipewa kipaumbele cha kwanza na Maaskofu wa Amerika ya Kusini katika mkutano uliofanyika huko Puebla kunako mwaka 1979. Mwenyeheri Oscar Romero akaonesha kwamba: umaskini ni dhambi katika mwelekeo wake wa kitaalimungu na dhamana inayopaswa kufanyiwa kazi na wadau mbali mbali kwani unadhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Huu ndio ukweli ambao Baba Mtakatifu Francisko anatamani kuuona katika Kanisa la Kristo, yaani Kanisa maskini kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mwenyeheri Oscar Romero ni kielelezo cha askofu ambaye ni mhudumu wa Injili ya Yesu Kristo na chachu ya matumaini ulimwenguni. Katika mshikamano huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina limewaandikia Maaskofu wa El Salvador barua ya shukrani kwa Kanisa kumtangaza Askofu mkuu Oscar Romero kuwa Mwenyeheri. Kardinali Mario Aurelio Poli, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Buenos Aires, Jumamosi, tarehe 23 Mei 2015 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa upendo na ukarimu wake kwa Familia ya Mungu Amerika ya Kusini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.