2015-05-23 08:35:00

Waamini walei katika kulitegemeza Kanisa na kuyatakatifuza malimwengu!


Askofu Desiderius Rwoma wa Jimbo Katoliki Bukoba, Tanzania, katika mahojiano maalum na Radio Vatican, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Sherehe ya Pentekoste kwa mwaka huu 2015 anapenda kuwashukuru na kuwapongeza waamini walei katika mchakato wa kulitegemeza Kanisa mahalia, kushuhudia imani yao pamoja na kuendelea kuyatakatifuza malimwengu, changamoto kubwa inayojikita katika kanuni maadili na tunu msingi za maisha ya Kikristo, kielelezo makini cha imani tendaji.

Askofu Rwoma anabainisha kwamba, waamini walei nchini Tanzania wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia ustawi wa Kanisa mahalia kwa hali na mali. Changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, wanajikita katika kudumisha na kuendeleza Injili ya Familia kwa njia ya malezi makini yatakayowasaidia waamini kujenga utamaduni wa hofu ya Mungu, ili kuondokana na dhambi pamoja na nafasi zake. Kumong’onyoka kwa maadili na utu wema, kunawafanya watu wengi kutokuwa na hofu wala kinyaa cha kutenda dhambi.

Askofu Rwoma anasema, ulevi wa kupindukia unahatari sana katika ustawi, maendeleo na mfungamano wa maisha ya kifamilia. Ulevi umesambaratisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, zimeathiri malezi na makuzi ya watoto wengi, zimezitumbukiza familia katika umaskini wa hali na kipato. Watu wasikubali kutawaliwa na ulevi na kwamba, kuna nafasi ya watu kuachana na tabia hii na kuanza maisha mapya kwa kuwa na kiasi. Kwa njia hii wataweza kupata nafasi ya kusali, kuboresha maisha yao na kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Askofu Rwoma anawataka waamini walei kuwa kweli ni vyombo na wajenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano katika jamii kwa kukataa kutoa wala kupokea rushwa sanjari na kujikita katika kanuni maadili na utu wema. Kwa njia hii wanaweza kusaidia kuyatakatifuza malimwengu. Waamini kamwe wasiogope kushuhudia imani yao inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku na kamwe wasiwe na uchu wa mali, fedha na madaraka, mambo hatari yanayoendelea kusababisha majanga makubwa sehemu mbali mbali za dunia.

Kwa namna ya pekee kabisa Askofu Rwoma anawashukuru na kuwapongeza waamini walei nchini Tanzania kwa kuendelea kuchangia katika ujenzi wa kituo cha walei nchini Tanzana, Bakanja na kwamba, kituo hiki kitakamilika kwa jeuri ya waamini walei!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.