2015-05-22 09:31:00

Waamini wa dini mbali mbali: Dumisheni misingi ya haki, amani na maridhiano!


Viongozi wakuu wa Makanisa nchini Uingereza wanasikitishwa sana na mauaji, nyanyaso na dhuluma wanazofanyiwa Wakristo, sehemu mbali mbali za dunia. Taarifa na shuhuhuda mbali mbali kutoka Iraq, Iran, Misri, India, Pakistan na Indonesia zinaonesha kwamba, katika maeneo haya Wakristo wanateseka sana. Viongozi wakuu wa Makanisa wanawataka watu wote wenye mapenzi mema kuheshimu, kulinda na kutetea utakatifu wa maisha sanjari na kusaidia maboresho ya ustawi na maendeleo ya mwanadamu.

Viongozi hawa wanasema kwamba, imani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na inapaswa kumwilishwa katika maisha ya waamini kwa uhuru kamili pasi na shuruti. Kumbe, hii ni changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanajikita katika majadiliano yanayoheshimu na kuthamini misingi ya haki, amani na maridhiano.

Kwa namna ya pekee, viongozi wakuu wa Makanisa wanamkumbuka Askofu mkuu Oscar Romero, kutoka El Salvador, aliyeuwawa kutokana na chuki za kidini kunaki tarehe 24 Machi 1980. Viongozi hawa wanapenda kuungana na Familia ya Mungu nchini El Salvador kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa Mtumishi wa Mungu Askofu mkuu Oscar Romero kutangazwa kuwa ni Mwenyeheri, hatua muhimu kabla ya kutangazwa kuwa Mtakatifu ndani ya Kanisa Katoliki.

Askofu mkuu Oscar Romero ni kielelezo na ushuhuda makini wa watu ambao wameuwawa kikatili kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Viongozi wanawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali, wakati huu Kanisa linapofanya kumbu kumbu ya miaka thelathini na mitano tangu alipouwawa ili kuwakumbusha Wakristo kwamba, damu ya Wakristo inayoendelea kumwagika sehemu mbali mbali za dunia, ni mbegu ya Ukristo inayozikwa mioyoni mwa watu, itachanua kwa wakati wake na amani ambayo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu itachanua na kustawi katika miyo ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.