2015-05-22 10:05:00

Nigeria pambaneni kikamilifu na rushwa, ufisadi na udini: Saratani ya taifa


Askofu mkuu Ignatius Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, hivi karibuni ameitaka Familia ya Mungu nchini Nigeria kuondokana na ubinafsi pamoja na uchoyo, tayari kuelekeza nguvu zao kwa ajili ya kutafuta na kudumisha mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu. Watu wanataka kuona mchakato wa utawala bora unaimarishwa na kudumishwa, kama kielelezo cha mabadiliko katika mawazo na mitazao ya watu wote wa Nigeria. Rushwa, misiamo mikali ya kidini ni saratani inayoendelea kuwatendea sana wananchi wa Nigeria katika ujumla wao.

Askofu mkuu Kaigama anasema kwamba, umefika wakati kwa wananchi wa Nigeria kuondokana na mambo ya: Ukabila, udini, umajimbo kwa kujikita katika ujenzi wa umoja na mshikamano wa kitaifa, dhamana inayopaswa kutekelezwa na wananchi wa Nigeria, kwa kutambua kwamba, wanawajibika kuwa ni sauti ya kinabii. Wakristo kwa namna ya pekee kabisa, wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba wanashiriki katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.

Waamini wanapaswa kutambua kwamba, wao ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa; watende yote kwa sifa na utukufu wa Mungu. Ili kujikita katika ujenzi na ustawi wa Nigeria, wananchi hawana budi kuondokana na chuki na uhasama usiokuwa na mashiko wala maendeleo kwa watu na badala yake, kila mwananchi ajifunge kibwebwe kwa ajili ya maendeleo yake binafsi, umoja, upatanisho na mshikamano wa kitaifa. Dhana ya kudhaniana vibaya inakwamisha mchakato wa maendeleo endelevu.

Askofu mkuu Ignatius Kaigama ametoa changamoto hizi, wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumweka wakfu Askofu msaidizi Denis Chidi Isizoh wa Jimbo kuu la Onitsha, Nigeria ambaye hivi karibuni aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko. Kabla ya uteuzi huu Askofu msaidizi Denis Chidi Isizoh alikuwa ni afisa mwandamizi katika Baraza la Kipapa la Utamaduni.

Ibada ya Misa Takatifu imeongozwa na Kardinali Francis Arinze, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Ibada, Nidhamu na Sakramenti za Kanisa. Imehudhuriwa na waamini pamoja viongozi mbali mbali wa Kanisa na Serikali kutoka ndani na nje ya Nigeria. Askofu mkuu Augustine Kasujja, Balozi wa Vatican nchini Nigeria ameshiriki kikamilifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.