2015-05-22 07:59:00

Mkutano wa kimataifa wa kupambana dhidi ya mauaji na nyanyaso kwa Wakristo


Kila mwaka kuna matukio yanayoonesha kunajisiwa kwa Makanisa na uharibifu mkubwa unaofanywa dhidi ya maeneo ya vielelezo vya imani na ibada; kuna mauaji ya Wakristo yanayoendelea sehemu mbali mbali za dunia, bila kuwasahau viongozi wao. Haya ni mambo ambayo yamejadiliwa kwenye mkutano wa pili kimataifa kwa ajili ya ushirikiano na mshikamano wa kimataifa katika masuala ya usalama Barani Ulaya, OSCE. Lengo la mkutano huu ni kuzuia na kupambana vikali na hali ya kutowavumilia pamoja na kuwatenga Wakristo.

Mkutano huu ambao ulikuwa unafanyika mjini Vienna, Austria umehudhuriwa na viongozi wa Serikali pamoja na Mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayoendelea kusimama kidete kupambana na ubaguzi na mauaji dhidi ya Wakristo. Mkutano huu umefanyika katika awamu kuu tatu kwa lengo la kudhibiti tabia hii chafu isiendelee kutanuka. Itakumbukwa kwamba, mkutano wa kwanza wa OSCE ulifanyika mjini Roma, kunako mwaka 2011.

Tangu wakati huo, kumekuwepo na ongezeko kubwa la vitendo vya kibaguzi na mauaji ya Wakristo si tu Barani Afrika, Asia na Mashariki ya Kati, bali hata Barani Ulaya. Takwimu zinaonesha kwamba, Wakristo ni kati ya makundi makubwa ya kidini yanayoendelea kunyanyaswa na kudhulumiwa. Hapa wajumbe wanasema, kuna dalili pia za mauaji ya kimbari yanayofanywa kwa misingi ya udini. Mauaji ya kimbari hayajaanza kujitokeza katika nchi za OSCE kwa sasa!

Monsinyo Janus Urbanczyk, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa nchi za OSCE ameongoza ujumbe wa Vatican kwenye mkutano huo. Wajumbe wamepembua kwa kina na mapana na hatimaye, kutofautisha kati imani ya kidini na kile ibada ya hadhara inayooneshwa na waamini. Kila mtu ana uhuru wa kuamini na kufanya ibada katika nyumba za Ibada. Wananchi wanapaswa kujenga utamaduni wa majadiliano ya kidini ili kuvumiliana na kwamba, tabia ya kukosa kwa maridhiano kati ya watu ni chanzo cha kinzani, vurugu na vita.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.