2015-05-19 16:06:00

Changamoto katika maisha na utume wa Kanisa nchini Italia!


Baada ya Baba Mtakatifu Francisko kufungua maadhimisho ya mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI kwa hotuba iliyosheheni changamoto za kichungaji, Jumanne, tarehe 19 Mei 2015, Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia alikazia kwa namna ya pekee maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, Mwaka wa Watawa Duniani, Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia, Kongamano la Kanisa Kitaifa pamoja na kilio cha watu wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia kutokana na majanga asilia, vita, nyanyaso na madhulumu.

Kardinali Bagnasco anawaalika Maaskofu kwa namna ya pekee kupokea maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kama zawadi kubwa kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko inayowahamasisha kuwa na huruma kama Mwenyezi Mungu alivyo na huruma. Kiwe ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani kwa kukimbilia huruma wakati wa kufungua malango ya Makanisa ya Jubilei. Kiwe ni kipindi cha kujikita katika mchakato wa kutafuta na kudumisha misingi ya haki na amani sanjari na kumwilisha imani katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Iwe ni fursa ya kuamsha dhamiri nyofu, ili kutoka kimasomaso ili kupambana na umaskini wa hali na kipato na kwamba, Sakramenti ya Upatanisho, iwe ni dira na mwongozo wa waamini katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Hii ni nafasi pia kwa Familia ya Mungu nchini Italia, kumshukuru Mungu kwa ajili ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 200 ya kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Bosco. Onesho la Sanda Takatifu iwe ni fursa ya kuamsha tena matumaini yanayobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Yesu.

Kardinali Bagnasco anabainisha kwamba, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia, ni fursa ya kuendeleza majadiliano ya kina yanayojikita katika tafakari, sala, uzoefu na mang’amuzi kuhusu Injili ya Familia, ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto nyingi, ili kupata msimamo na mwelekeo wa pamoja. Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, inapaswa kuiga mfano wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu; kwa kuheshimu na kuthamini tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; kwa kuenzi na kudumisha ukweli na upendo katika maisha ya ndoa na familia. Tarehe 3 Oktoba 2015, Familia ya Mungu nchini Italia, itafanya mkesha wa sala kwa ajili ya kuombea Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Kardinali Bagnasco katika hotuba yake elekezi amewashukuru na kuwapongeza wahusika wote wanaendelea kuchakarika ili kufanikisha maadhimisho ya Kongamano la Kikanisa Kitaifa litakalofanyika mjini Firenze, kuanzia tarehe 9 hadi 13 Novemba 2015. Hii ni fursa kwa Kanisa nchini Italia kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano na tamaduni mbali mbali, ili kweli kama viongozi wa Kanisa waendelee kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa; katika uhuru na ukweli; katika imani na fikara za mwanadamu; kwa njia ya ushuhuda na majadiliano yanayoonesha imani tendaji.

Kardinali Angelo Bagnasco amewashirikisha Maaskofu wenzake mateso na mahangaiko ya watu sehemu mbali mbali za dunia kutokana na majanga asilia kama yalivyotokea nchini Nepal na jinsi ambavyo Kanisa limeonesha mshikamano wa upendo na udugu. Amekumbusha mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Ukraine, miaka mia moja iliyopita , lakini walimwengu hawataki kukubali kwamba, haya ni mauaji ya kimbari, changamoto ya kujikita katika misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Bado kuna Wakristo wanaoendelea kuuwawa kikatili, kunyanyaswa na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Kanisa Katoliki nchini Italia, Jumamosi, tarehe 23 mei 2015, katika Mkesha wa Siku kuu ya Pentekoste, litasali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Wakristo sehemu mbali mbali za dunia wanaoendelea kumwaga damu yao kama mbegu ya imani inayozikwa katika mioyo ya watu, itachanua kwa wakati muafaka.

Kardinali Bagnasco anasema kwamba, Familia ya Mungu nchini Italia, inaendelea kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa mbali mbali. Bado kuna idadi kubwa ya wananchi hasa vijana hawana ajira na kwamba, uchumi bado unakua kwa kusuasua, changamoto na mwaliko kwa wanasiasa, wachumi na watunga sera kujikita katika mikakati itakayosaidia kufufua uchumi. Kuna idadi kubwa ya wahamiaji na wakimbizi wanaoendelea kufa maji kwenye Bahari ya Mediterrania: hawa ni wale wanaokimbia vita, njaa, dhuluma na nyanyaso, wanapaswa kusaidia na kuonjeshwa ukarimu.

Ulevi wa kupindukia miongoni mwa vijana sanjari na mchezo wa kamari ni kati ya majanga makubwa yanayoendelea kuwaandama wananchi wa Italia. Hapa kuna haja ya kuwekeza katika elimu makini, majiundo safi na bora kutoka katika familia. Mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya familia zinapaswa kuimarishwa zaidi pamoja na kuendelea kuwafunda wanandoa kutambua tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Talaka za chapu chapu zilizopitishwa hivi karibuni na Bunge la Italia ni hatari kwa ustawi na maendeleo ya familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.