2015-05-18 07:41:00

Kumbu kumbu ya Vita kuu ya Pili ya Dunia: Changamoto: amani na uhuru!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, CCEE pamoja na Shirikisho la Makanisa Ulaya, CEC, hivi karibuni yalifanya mkutano wa pamoja na hatimaye, kuchapisha tamko la pamoja linalokazia umuhimu wa kulinda na kuheshimu uhuru, amani na maridhiano kati ya watu kama njia muafaka ya kuwaenzi wananchi waliojisadaka kwa ajili ya kupigania uhuru kwa mafao ya wengi.

Wakati huu Jumuiya ya Kimataifa inapoendelea kufanya kumbu kumbu ya miaka 70 tangu kusitishwa kwa Vita kuu ya Pili ya Dunia, kuna haja kwa wananchi Barani Ulaya, kusimama kidete dhidi ya utamaduni wa kifo. Mapambano ya kutafuta haki na uhuru yalipelekea kuzaliwa kwa haki msingi za binadamu ambazo zinapaswa kukuzwa na kudumishwa na wapenda amani sehemu mbali mbali za dunia. Lakini, ikumbukwe kwamba, uhuru kimsingi unakwenda sanjari na wajibu, kwani hakuna uhuru pasi na wajibu wanakumbusha viongozi wa Makanisa.

Bara la Ulaya kwa sasa linatembea katika uvuli wa historia yake, changamoto kubwa kwa sasa ni kupyaisha mwono, mwelekeo na vipaumbele vitakavyosaidia kuenzi uhuru kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi. Hapa kuna haja ya kuwa na mwono wa Kikristo kuhusiana na uhuru, kwani mwanadamu ameumbwa huru kabisa kadiri ya mapenzi ya Mungu. Yesu Kristo anawahamasisha wafuasi wake kutumia uhuru wao kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu.

Uhuru wa kweli ni ule ambao unaheshimu na kuthamini pia uhuru wa wengine na ambao unajikita katika fadhila ya ukweli na wala si kwa ajili ya kuridhisha tamaa na maonjo ya watu binafsi. Viongozi wa Makanisa wanataka Jamii ikazie uhuru unaoheshimu utu wa binadamu na kukataa nyanyaso, dhuluma na mauaji kwa misingi ya kidini. Wanataka uhuru ambao utasaidia kuokoa maisha ya wahamiaji na wakimbizi wanaoendelea kufa maji huko kwenye Bahari ya Mediterrania, kwa kusitisha vita na majanga mengine, ili waweze kuishi kwa amani katika nchi zao.

Viongozi wa Makanisa wanataka uhuru unaonesha mshikamano ili kuondokana na mawazo mepesi mepesi yanayowabagua wengine sanjari na kuwatumbukiza katika biashara ya utumwa mamboleo na viungo vya binadamu, mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanataka uhuru unaoheshimu kazi ya uumbaji kama zawadi kutoka kwa Mungu kwa ajili ya mafao ya wengi; uhuru unaokuza na kujenga matumaini badala ya kuwakatisha wananchi tamaa ya maisha.

Viongozi wa Makanisa wanasema, wanapenda kujikita katika uhuru unaoiwezesha mioyo na akili zao kuwa huru, tayari kuganga na kuponya madonda ya chuki, uhasama na utengano, kwa kujikita katika matumaini ya haki, amani na maridhiano. Wananchi wanakumbushwa kwamba, wao wanaitwa kuwa huru, lakini uhuru wao usiwatumbukize katika tamaa ya mwili, bali wawe ni vyombo vya huduma ya upendo, kwa Mungu na jirani.

Hivi ndivyo Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya na Shirikisho la Makanisa Ulaya yanavyohitimisha tamko lao pamoja, wakati huu Jumuiya ya Kimataifa inapoendelea kufanya kumbu kumbu ya miaka 70 tangu kusitishwa kwa Vita kuu ya Pili ya Dunia, huo ukawa ni mwanzo wa ukursa mpya katika maisha ya watu wengi duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.