2015-05-16 09:42:00

Mitandao ya Kijamii ni muhimu sana katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya


Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Kupaa Bwana mbinguni sanjari na Siku ya 49 ya Upashanaji habari ulimwenguni ambayo kwa mwaka 2015 inaongozwa na kauli mbiu “Mawasiliano katika familia: mazingira muhimu yanayowakutanisha watu katika majitoleo ya upendo” maneno yanayofumbata kiini cha ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya Upashanaji habari ulimwenguni. Changamoto hii imepembuliwa kwa kina na mapana na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, katika semina iliyoandaliwa kwa ajili ya wakurugenzi wa idara za mawasiliano ya jamii, kutoka katika nchi za AMECEA.

Mama Kanisa anachangamotishwa kwa namna ya pekee kuhakikisha kwamba, anajikita katika matumizi ya mitandao ya kijamii, ili kuwatangazia watu wanaoishi katika ulimwengu wa mitandao, Habari Njema ya Wokovu na kwa namna ya pekee, kukutana na kuzungumza na vijana kwenye mitandao ya kijamii, kwani huko wameweka maskani yao! Waswahili wanasema, hakieleweki kitu pasi na mitandao ya kijamii!

Askofu Charles Kasonde, Mwenyekiti wa Idara ya mawasiliano AMECEA anabainisha kwamba kuna mambo kadhaa ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi: kwanza kabisa na kuunda jukwaa la majadiliano litakalosaidia uundwaji wa miundo mbinu ya mawasiliano pamoja na kuwa na uhakika wa teknolojia inayotakiwa, ili kuibua mbinu mkakati unaojikita katika azma ya Kanisa ya Uinjilishaji mpya pamoja na kushirikishana taarifa mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa.

Kwa upande wake Padre Fabian Pikiti, katibu wa Idara ya shughuli za kichungaji kutoka AMECEA anabainisha kwamba, ulimwengu mamboleo unajikita katika maendeleo ya sayansi na teknolojia hivyo, Kanisa halina budi kuhakikisha kwamba, linasoma alama za nyakati ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya kwa kuwa na matumizi sahihi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari. Watu watangaziwe Habari Njema ya Wokovu, ili waweze kupata wokovu na maisha ya uzima wa milele.

Teknolojia ya mawasiliano, halina budi kulisaidia Kanisa kutekeleza dhamana hii nyeti katika maisha na utume wake hapa duniani. Mama Kanisa kwa namna ya pekee, hana budi kuhakikisha kwamba, anaelekeza jicho lake la imani na matumaini kwa vijana wa kizazi kipya ambao wanaogelea kwenye mitandao ya kijamii usiku na mchana, huko wamejenga “maskani na vijiwe” vinavyowakutanisha. Kanisa halina budi kujiwekea mikakati ya kuwafuta huko huko waliko, ili kuwatangazia Injili ya Furaha, Imani na Matumaini, tayari kuwasaidia katika hija ya maisha yao: kiroho na kimwili.

Semina hii imewashirikisha wajumbe kutoka  katika nchi za AMECEA ambazo ni Eritrea, Ethiopia, Kenya, Malawi, Sudan, Tanzania, Uganda na Zambia. Lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Idara za mawasiliano ya jamii kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu wa AMECEA, tayari kuchangia zaidi katika mchakato wa mawasiliano ndani na nje ya AMECEA, kama sehemu ya utekelezaji wa dhamana ya Uinjilishaji mpya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CANAA.








All the contents on this site are copyrighted ©.