2015-05-07 11:18:00

Wakristo shikamaneni ili kukabiliana na changamoto katika maisha!


Kamati ya pamoja kati ya Shirikisho la Mabaraza ya Makanisa Ulaya, CEC na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, CCEE ni ushuhuda wa hija ya kiekumene inayopaniwa na Makanisa Barani Ulaya, ili kuganga na kuponya madonda ya utengano yaliyosababisha Wakristo kusigana na kugombana. Leo hii mambo ni tofauti kabisa, kwani kwa neema ya Mungu, Makanisa Barani Ulaya yameanza mchakato wa upatanisho na amani, jitihada ambazo kwa namna ya pekee zilianza kujionesha kunako mwaka 2001. Hiki ni kielelezo cha matumaini ya umoja unaoonekana ingawa bado kuna njia ndefu inayopaswa kutekelezwa, ili Wakristo waweze kuwa na umoja kamili.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 7 Mei 2015 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Tume ya pamoja ya Shirikisho la Mabaraza ya Makanisa Ulaya pamoja na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya. Licha ya magumu ambayo yanajionesha lakini Tume hii ni sehemu ya mchakato wa upatanisho na umoja ambao Yesu anawataka wafuasi wake wautekeleze kwa kujikita katika upendo na ukweli.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Waraka wao kuhusiana na majadiliano ya kiekumene wanasema kwamba,  utengano huo hupingana wazi na mapenzi ya Kristo, nao ni kikwazo kwa ulimwengu na hudhuru tendo takatifu la kuhubiri Injili kwa kila kiumbe na hata wakati mwingine misimamo ya Kanisa kwa masuala ya kiutu na kimaadili. 

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wajumbe wataweza kukutana mara kwa mara kwa ajili ya tafakari ya kina katika mwanga wa Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa. Kristo ambaye ni Adam mpya, akilifunua Fumbo la Baba na upendo wake, hudhihirisha kikamilifu kwa binadamu, binadamu alivyo, na kumjulisha wito wake mkuu. Wakristo wanaweza kupata majibu ya pamoja kwa maswali wanayoulizwa na walimwengu. Kwa kuwa karibu na Kristo, wanaweza kushikamana na kujenga umoja.

Makanisa Barani Ulaya yanakabiliana na changamoto ambazo zinaweza kushughulikiwa kwa pamoja, kwa kuwa na sauti moja, kuhusu uhuru wa kuabudu na maridhiano kati ya waamini wa dini mbali mbali. Changamoto ya wahamiaji na wakimbizi inaweza pia kushughulikiwa kwa njia ya ushirikiano kati ya Makanisa, kwani hawa ni watu wanaokimbia kutoka katika vita, madhulumu na maafa. Makanisa yanaweza kushirikiana kujenga mshikamano na ukarimu; kwa kuombea utulivu, kudumisha majadiliano na amani katika maeneo ya vita.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.