2015-04-28 12:08:00

uhusiano wa maadili, mabadiliko ya tabia nchi na maendeleo endelevu


Hapa Vatican , Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya elimu ya sayansi,Jumanne 28 Aprili 2015,  imekuwa mwenyeji wa warsha muhimu, iliyo chambua kwa kina uhusiano kati ya maadili ya kidini , mabadiliko ya tabia nchi na Maendeleo  endelevu, katika lengo la kulinda mazingira ya dunia na kukuza ubinadamu.Kati ya watu mashuhuri walioshiriki katika warsha hii ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa , bwana Ban Ki-moon,  ambaye  hotuba yake, imeitaja Mada mbiu kuu ya warsha kuwa  jambo muhimu la kidharura katika  nyakati zetu.

Kiongozi huyo wa Kimataifa,  ametoa shukurani zake za dhati kwa Papa Francisco na kwa viongozi wa kidini na sayansi, waliofika katika mkutano huu ambamo wameonyesha utambuzi wao katika haja ya kidharura ya kukuza maendeleo endelevu na wakati huohuo,  kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.  Na kwamba yeye na Papa Francisco hivi karibuni walipata muda wa kujadili  kwa mapana  zaidi , masuala mbalimbali yanayoikabili dunia kwa  wakati huu.Bwana Ban Ki-Moon ameendelea kusema, kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na kurekebisha  madhara yake ni vipengere muhimu katika kutokomeza umaskini uliokithiri, kupunguza ukosefu wa usawa na usalama sawia sambamba na maendeleo endelevu ya kiuchumi. Na hivyo akaitaja  changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi, kuwa  tatizo kubwa  la nyakati zetu,  linalohitaji utendaji makini kwa ajili ya maendeleo endelevu.


Aliendelea kujali kwamba, mabadiliko ya tabia nchi , pia  yana husishwa na afya ya umma, upatikanaji wa chakula na maji salama, uhamiaji, amani na usalama. Na hivyo ni  suala la kimaadili. Ni suala la haki za kijamii, haki za binadamu na maadili  msingi. Kwa  hiyo binadamu anao wajibu msingi katika kulinda na kudumisha  mfumo tete wa mtandao wa maisha ya dunia hii, kwa ajili ya kizazi hiki na vizazi vijavyo. Ndiyo maana  inakuwa ni muhimu sana kwa makundi ya kidini  kuwa wazi katika suala hili  na hasa katika mtazamo wa upatanifu wake na sayansi.   Katika mabadiliko haya ya tabia nchi , maoni ya Sayansi na dini hayatofautiani, bali  hakika yanapatana.

Kwa maoni hayo Katibu Mkuu Ban  , amehimiza wote  kwa pamoja,  kutoa maelezo bayana ya kweli, kisayansi na  maoni ya kidini , juu ya  mabadiliko ya tabia nchi, akisema sasa  si suala la mashaka mashaka  bali ni  tatizo kubwa na  wazi kwamba,  mabadiliko ya tabia nchi yanayotokea  sasa , sababu kubwa , ni matendo hasi  binadamu . Ukweli huo, unaozingatiwa  sasa na Jopo la Kimataifa juu ya Mabadiliko ya Tabia nchi na Taasisi kubwa za kisayansi za kila serikali duniani, ikiwa ni pamoja na  Taasisi ya Vatican ya Elimu ya Sayansi . Na hivyo jibu la Kimataifa kiujumla linatakiwa kutolewa katika misingi ya uadilifu mzima wa ulimwengu.

Katibu Mkuu Ban Kimoon amesisitiza, mabadiliko ya tabia nchi yaathiri watu wote, ingawa si katika hali za kulingana.  Alieleza kwa kutaja wale ambao, wanakabiliwa na hali ngumu zaidi , ingawa  hawahusiki sana na utendaji  mbovu wa binadamu unaosababisha hali hiyo mbaya , hasa mataifa maskini na watu wanyonge katika jamii . Duniani kote anasema , kunashuhudiwa jinsi mafuriko, ukame, kupanda kwa viwango vya bahari na dhoruba vinavyozidi kuongezeka na kusababisha madhara ya kutisha, ikilazimu familia  nyingi kuhamia maeneo mengine , mara nyingi katika hatari kubwa.

Alieleza na kurejea maneno ya Papa Francisco kwamba , dunia inahitaji kuyatazama matatizo haya kwa jicho la imani, katika uhusiano kati ya mazingira asilia na hadhi ya  utu wa mtu na kwamba walio wanyonge zaidi ni lazima, wawe kiini cha wazo la majadiliano ya mwaka huu,  wakati serikali zinapotafuta  jibu la kimataifa katika  kukabiliana na mabadiliko hayo ya tabia nchi na ujengaji  wa mfumo mpya kwa ajili ya maendeleo endelevu.

 Katibu Mkuu ameonyesha matumaini yake kwamba, ,  Malengo mapya  ya Maendeleo ya endelevu, yatakayo pitishwa mwezi  Septemba, yataweza kuwa na jibu adilifu , lenye kuiweka jamii na mazingira, sambamba na malengo ya kiuchumi, ili kwamba, kutokomeza umaskini uliokithiri, na  kusitisha ubaguzi wa kijamii dhidi ya makundi  dhaifu na wanyonge, na ulinzi wa  mazingira, zinakuwa tunu msingi katika ukamilifu wa mafundisho ya dini zote kuu. 








All the contents on this site are copyrighted ©.