2015-04-18 10:23:00

Uchaguzi mkuu Togo: Kanisa kutopeleka watazamaji wakati wa uchaguzi


Baraza la Maaskofu Katoliki Togo limeamua kwamba, halitapeleka watazamaji wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu wa Wabunge na Rais unaotarajiwa kufanyika nchini humo tarehe 25 Aprili 2015 kama kielelezo kwa Maaskofu kutoridhishwa na hatua za Serikali kutofanya mageuzi makubwa yaliyokuwa yamebainishwa na wananchi wa Togo. Serikali kwa miaka mitano imeshindwa kuchapisha taarifa rasmi za uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo kunako mwaka 2010, uliogubikwa na malalamiko mengi.

Serikali imeshindwa pia kutekeleza mapendekezo 68 yaliyotolewa na Tume ya haki, amani na upatanisho, ambayo pamoja na mambo mengine, ilikuwa inaitaka Serikali kulipa fidia watu walioathirika kutokana na machafuko ya kisiasa na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu nchini Togo. Serikali ilikuwa imeshauriwa kuimarisha utawala bora unaozingatia kanuni maadili, sheria na haki msingi za binadamu; mambo ambayo hayajatekelezwa hadi wakati huu na kwamba, Serikali ilikuwa ichapishe sera na mikakati ya upatanisho nchini Togo, ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa; mambo yote haya yamepuuzwa! Kwa mantiki hii, Maaskofu hawaoni sababu ya Kanisa kupeleka watazamaji kwenye uchaguzi mkuu nchini humo.

Maaskofu wanasikitika kusema kwamba, Serikali imeshindwa kutekeleza mabadiliko ya Katiba kama ilivyokuwa imekubaliwa kunako mwaka 2006, kama njia ya kudhibiti machafuko ya kisiasa yasijirudie tena kama ilivyojitokeza kunako mwaka 2005 wakati wa uchaguzi mkuu. Itakumbukwa kwamba, uchaguzi huu ulitarajiwa kufanyika tarehe 15 Aprili 2015, lakini ukasogezwa mbele kutokana na ushauri uliotolewa na Jumuiya Uchumi Afrika Magharibi, ECOWAS, CEDAO. Lengo ni kutafuta suluhu na ufumbuzi wa baadhi ya matatizo na changamoto ambazo zimebainishwa na viongozi wa upinzani, hususan kuhusiana na Daftari la kudumu la Wapiga kura.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.