2015-04-18 11:09:00

Rais Mattarella wa Italia: Mshikamano, uhuru wa kuabudu, Jubilee kuu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 18 Aprili 2015 amekutana na kuzungumza na Rais Sergio Mattarella wa Italia ambaye amemtembelea rasmi mjini Vatican, baada ya kuchaguliwa hivi karibuni kuwaongoza wananchi wa Italia. Katika hotuba yake, Rais Mattarella amemshukuru Baba Mtakatifu kwa maneno na ushuhuda unaonesha mahusiano ya karibu kati ya Vatican na Italia. Wananchi wa Italia wameendelea kuonesha upendo mkubwa kutokana na ukweli kwamba, Papa Francisko anawajali na kuwapenda, changamoto ya kuendelea kujenga na kuimarisha mshikamano katika nyakati mbali mbali za maisha ya wananchi wa Italia.

Kuna uhusiano wa karibu kati ya Vatican na Serikali ya Italia katika mahusiano yanayojikita kwenye medani mbali mbali za maisha kama vile: kijamii, kiuchumi na kisiasa; mambo ambayo kimsingi yanajikita katika historia na demokrasia nchini Italia na Ulaya katika ujumla wake. Italia inampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa mafundisho yake makuu yanayojikita katika: fursa za ajira, haki na amani; maendeleo endelevu ya binadamu; utu na heshima ya binadamu na kwamba, kwa njia ya mafundisho haya, wananchi wa Italia wanajisikia kuwa karibu sana na Baba Mtakatifu.

Baba Mtakatifu tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki anasema Rais Mattarella, ameguswa sana na matatizo na matumaini ya wananchi wa Italia; changamoto na matatizo ya kimataifa yanayosababishwa na umaskini wa hali na kipato; nyanyaso na madhulumu ya kidini, ukame na baa la njaa pamoja na vita na matokeo yake ni wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta hifadhi nchini Italia na Ulaya katika ujumla wake. Serikali ya Italia imekabiliana na changamoto zote hizi kwa moyo wa ukarimu, lakini linaitaka Jumuiya ya Ulaya kusaidia mchakato wa kuokoa maisha ya watu wanaokufa maji kwenye Bahari ya Mediterrania pamoja na kuwajengea watu matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Rais Sergio Mattarella anasema kwamba, wananchi wa Italia wanakabiliwa na changamoto za ukosefu wa fursa za ajira na umaskini, hali ambayo inaitaka Serikali kuwa ni sera na mikakati mipya ya kiuchumi na kijamii kwa kutoka kipaumbele cha kwanza kwa mahitaji ya binadamu na familia katika ujumla wake sanjari na kujenga utamaduni wa mshikamano badala ya kumezwa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Serikali inaendelea kubainisha sera na mikakati makini ili kupambana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Serikali inalipongeza Kanisa kwa kusaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Rais Sergio Mattarella anabainisha kwamba, Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilee ya huruma ya Mungu, itakuwa ni fursa ya kufanya tafakari ya kina mintarafu haki, amani na mshikamano; ili kuimarisha mahusiano kati ya watu wa mataifa katika masuala ya kiuchumi na kijamii, ili kudhibiti kinzani na migawanyiko ya kijamii. Mwaka wa Jubilee ya huruma ya Mungu, iwe ni nafasi ya kukoleza majadiliano ya kidini kati ya Waislam, Wayahudi na waamini wa dini mbali mbali, ili kukuza na kuimarisha uhuru wa kidini, mambo msingi katika Katiba ya Italia. Mauaji, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia ni mambo ambayo kamwe hayawezi kukubalika na wapenda haki na maridhiano ndani ya jamii.

Kumbe, anasema Rais Mattarella kuna haja ya kuimarisha majadiliano ya kidini ili kuondokana na tabia ya kutaka kulipizana kisasi. Italia itaendelea kujikita katika mchakato wa ushirikiano wa kimataifa na ujenzi wa misingi ya amani ya kweli duniani. Utunzaji bora wa mazingira, ugawaji sawa wa rasilimali ya nchi na onesho la chakula kimataifa huko Milano, Expo 2015 ni mambo ambayo Italia na Vatican wanaendelea kuyapatia kipaumbele cha pekee katika medani za kimataifa. Rais Sergio Mattarella wa Italia anahitimisha hotuba yake kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa kumwalika rasmi ili aweze kutembelea Ikulu ya Italia, kama sehemu ya mchakato wa kuendeleza mahausiano kati ya Serikali ya Italia na Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.