2015-04-18 09:51:00

Papa :Unyenyekevu wa Mkristo si kujidhalilisha lakini upendo


Baba Mtakatifu Francisko, anashauri watu wote,  kuepuka  kujibu hoja wakati wameghadhabishwa,  kwa kuwa kufanya hivyo,kuna uwezekano mkubwa wa kutoa jibu lisilo la haki. Anasema, daima tunapokasirishwa, ni vyema zaidi kukaa kimya kwanza, kujipa muda wa kutafakari kwa makini, jibu linalofaa kutolewa .  Na kwamba mtu kuwa mnyenyekevu haina maana ya kujidhalilisha,  na hasa inapokuwa hivyo kwa madhumuni ya kuyaiga maisha ya Yesu  Kristo mwenyewe.  Papa Francisco alieleza hilo wakati wa mahubiri yake  ya mapema Ijumaa , katika Kanisa dogo la Mtakatifu Marta la mjini Vatican.  Aliwataka Wakristo wote, kamwe kutopanda mbegu ya chuki na fitina , lakini kuutumia  muda wao mwingi,  katika tafakari za kugundua hisia za ndani  mwao wenyewe na mitazamo inayoweza kumpendeza Mungu, katika  maneno na matendo.

Papa alihoji iwapo inawezekana  kwa binadamu kukabiliana na hali ngumu na mateso  kwa  kutumia njia ya  Mungu? Alijibu, ndiyo, hiyo ndiyo  njia ya nyakati zote.  Kila wakati ni muda wa kupenyeza upendo wa Yesu katika maisha yetu kama ilivyoelezwa katika aya nyingi za Matendo ya Mitume..

Mafundisho ya Papa yalilenga katika  somo la siku kutoka Matendo ya Mitume , ambamo mnatajwa jinsi   Mfarisayo wa Gamalieli, wa Sanhedrin,  anavyowataka mitume waendelee kuhubiri  Injili, akiwa na imani kwamba, iwapo asili ya mahubiri yao ni binadamu yatakufa yenyewe na  iwapo yanatoka kwa Mungu yataendelea .  Watu hao wa Sanhedrin walikubali ushauri huo na hivyo kuamua kuyapa muda mahubiri ya Mitume . Papa aliwasifu watu hao kwamba hawakutoa jibu lenye kusukumwa na chuki  lakini walitulia na kuwa na muda wa kupima mambo . Papa alisema na hivyo ndivyo inavyotakiwa  kwa kila binadamu , katika kutoa majibu . Papa alisisitiza dawa ya chuki ya binadamu ni haki.

Papa amesisitiza, daima inafaa kwetu sote wakati tunapokuwa na mawazo maovu juu ya wengine , au hisia mbovu kwa wengine, tunapokuwa tumejawa na roho ya kutaka kutenda kwa ukatili au kulipiza kisasi , tunapozongwa na chuki kwa wengine , tusijiachie kumezwa na hayo , lakini tupate muda wa kutafakari juu ya hilo. Muda wa kusawazisha mawazo na kuyaweka katika mtazamo chanya wa maelewano. Kutoa  nafasi ya kuona mambo kwa haki zaidi, badala ya kutoa  jibu la papo kwa papo kwa  ghadhabu.  Papa anaonya,  hakika kutoa jibu ukiwa katika hali za  hasira, huongoza katika utendaji usiokuwa wa haki.  Na hivyo inakuwa ni kujiumiza wewe mwenyewe pia.

Papa alieleza na kutaja majivuno na kiburi huongoza katika nia mbovu za kutaka kuangamiza wengine .Lakini unyenyekevu hata kudhalilishwa , humwongoza mtu kwenye unyenyekevu kama ule wa Yesu. Bahati mbaya kwetu mara nyingi hatufikiri hivyo. Papa alieleza na kuzitazama hali halisi za wakati huu ambamo ndugu zetu wengi wake kwa waume wanauawa kwa ajili ya Imani yao kwa Kristo, wanateseka hadi kupoteza maisha yao wakiwa wamejawa na unyenyekevu na furaha ya kuwa Wakristo. Anasema wamekuwa na furaha ya kuruka kutoka katika kiburi na majivuno na kuingia katika njia ya uwazi wa moyo katika unyenyekevu , unyenyekevu usiopatikana bila ya kujishusha. Papa amesema hili ni jambo la ajabu ambalo ni gumu kulielewa kwa akili ya kibinadamu.Lakini hivyo ni neema tunayopaswa kuiomba kwa Mungu.

Ni Kuomba neema ya kumuiga  Kristo . Na si tu wafia dini wa leo wanao shuhudia hili , lakini ni kwa watu nyakati zote wake kwa waume  wanaoteseka kila siku na pia wale wanaoteseka kwa ajili ya mazuri ya familia zao , wale wanaofunga midomo yao , wasiozungumza mengi lakini wanakubali mateso hayo kwa sababu ya upendo wao kwa Kristo.  Huo ndiyo utakatifu wa Kanisa , hiyo ndiyo furaha yenye kumpa mtu unyenyekevu.  Furaha hiyo ya ndani, humfanya mtu  kujisikia yuko njiani pamoja na Yesu.  








All the contents on this site are copyrighted ©.