2015-04-17 10:45:00

Utume kwa vijana: Elimu na Uinjilishaji ni chanda na pete!


Kardinali Zenon Grocholewski, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la elimu Katoliki anasema, katika mchakato wa elimu, haitoshi kuwapatia vijana wa kizazi kipya ujuzi na maarifa, bali kuhakikisha kwamba, vijana hawa wanatumia vyema elimu, ujuzi na maarifa waliyojipatia wakati wakiwa shuleni kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi. Elimu iwasaidie vijana kuwa watu wema zaidi badala ya kuharibiwa na kuwa watu ovyo na wasumbufu ndani ya jamii.

Hii ni changamoto ambayo ameitoa hivi karibuni wakati alipokuwa anachangia mada kwenye kongamano la shughuli za kichungaji kwenye vyuo vikuu Barani Ulaya, lililokuwa linafanyika mjini Lodz, Poland. Mchakato wa elimu unaotolewa na Kanisa hauna budi kuhakikisha kwamba, unajikita katika maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, hii ni kati ya mikakati mitano inayopewa kipaumbele cha kwanza na Kanisa katika huduma za kichungaji kwenye vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu.

Wanafunzi wafundwe kuwa raia wema na wanaowajibika kwani kukengeukwa na kumong’onyoka kwa maadili na utu wema ni mambo ambayo yamekuwa ni chanzo kikuu cha majanga katika jamii nyingi duniani. Kumbe, Kanisa halina budi kuwekeza katika kanuni maadili, ili kuwafunda viongozi watarajiwa waweze kuwajibika barabara na kuendelea kuwa ni mwanga na matumaini ya jamii wanayoihudumia. Kanuni maadili ni muhimu sana katika majiundo makini ya binadamu katika misingi ya ukweli, uwazi na uwajibikaji makini.

Vijana wa kizazi kipya hawana budi kupewa elimu ya maisha ya kiroho ili kutambua ukuu wa Mungu na kutenda kwa busara badala ya kutumbukia katika dhana ya utepetevu wa mawazo na mmong’onyoko wa kimaadili kwa kisingizio cha uhuru binafsi. Majiundo makini ya kimaadili, kiroho na kitaaluma ni mambo msingi katika ukuaji na hatimaye, ukomavu wa mtu mzima.

Vijana wanapaswa pia kufundwa katika misingi ya fadhila ya upendo inayowajalia nguvu ya kutenda mema kwa ajili ya mafao na ustawi wa jirani zao, sanjari na kuwekeza katika mikakati ya kuimarisha tunu msingi za maisha ya kitamaduni na kiroho, ili kujenga majadiliano ya kina kati ya utamaduni na imani, ili kusaidia mchakato wa utamadunisho. Haya ni mambo msingi ambayo Papa Yohane Paulo II alikazia katika maisha na utume wake. Lengo ni kuwawezesha vijana kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Yesu Kristo Mkombozi wa dunia. Yesu ni njia, ukweli na uzima na utilimilifu wa matamanio ya binadamu.

Mchakato wa utamadunisho uwasaidie watu kutambua tunu msingi za kitamaduni zinazoweza kusaidia katika mchakato wa Uinjilishaji na kukataa mila, desturi na tamaduni zinazosigana na Injili ya Kristo. Waamini wanakumbushwa kwamba, Kanisa linawaalika kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji mpya kwa njia ya ushuhuda makini wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Na Padre  Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.  








All the contents on this site are copyrighted ©.