2015-04-17 15:55:00

Kardinali Roberto Tucci apumzishwa kwenye usingizi wa amani


Heri wafu wafao katika Bwana! Ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali wakati wa adhimisho la Misa Takatifu kwa ajili ya kumsindikiza Kardinali Roberto Tucci aliyefariki dunia hivi karibuni. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha adhimisho hili kwa Ibada ya maziko iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Ijumaa jioni tarehe 17 Aprili 2015. Ibada hii ya Misa takatifu imehudhuriwa na umati mkubwa wa Familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Roma.

Kardinali Tucci, Jumatano jioni tarehe 15 Aprili 2015 alifunga macho na kuingia katika usingizi wa amani, baada ya Mwenyezi Mungu kumkirimia maisha marefu na huduma iliyotukuka kama mtoto mpendwa wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Ni matumaini ya Kanisa kwamba, kwa maombezi ya Mtakatifu Inyasi, ataweza pia kufurahia maisha ya uzima wa milele, imani na matumaini kwa kila Mkristo. Wakristo wanapaswa kujiandaa kufa kifo chema! Ili kufanikisha tumaini hili, kuna haja ya kujitahidi daima kuishi ndani ya Kristo kwa kutambua kwamba, wanaishi na Mungu aliye hai na kuzamishwa kwa Mungu aliyekufa, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.

Waamini wajitahidi katika hija ya maisha yao kufa katika Kristo, kwani Yesu ni: njia, ukweli na uzima; maneno ya faraja ambayo yanapaswa kuwasindikiza wote walioguswa na msiba wa Kardinali Roberto Tucci. Kwa njia ya Kristo amefanikiwa kupata njia ya uhakika kuelekea nyumbani kwa Mwenyezi Mungu. Adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu, linapania kuiweka roho ya Marehemu Kardinali Tucci mikononi mwa Mwenyezi Mungu, kwa kumkirimia Ekaristi Takatifu kama masurufu ya njiani kuelekea mbinguni.

Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake za rambi rambi kwa Wayesuit anabainisha kwamba, Marehemu Kardinali Roberto Tucci analiachia Kanisa kumbu kumbu ya maisha ya mtu aliyejisadaka, kwa kuwa mahiri na mwaminifu katika wito wake wa kitawa. Ni kiongozi aliyekuwa makini kwa shida na mahangaiko ya wengine; Mchungaji mwaminifu kwa Injili ya Kristo na Kanisa lake; mtawa aliyejitahidi kufuata nyayo za Mtakatifu Inyasi wa Loyola kwa uaminifu mkubwa.  Huu ndio urithi ambao Kardinali Roberto Tucci ameliachia Kanisa! Mfano wa kuigwa na kuendelezwa na wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.