Baba Mtakatifu Francisko mapema Alhamisi hii, alikutana na kundi la Maaskofu wanaounda Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Kenya . Maaskofu hao wako katika hija yao ya kitume katika Kaburi la Mtakatifu Petro na Kiti Kitakatifu,tangu siku ya Jumatatu ya wiki hii na wanaikamilisha Ijumaa hii tarehe 17 Aprili 2015.
Akiongoza Msafara huo, Kardinali John Njue, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Nairobi, kwa niaba ya wenzake, alitoa hutoba fupi kwa Papa, kama ujumbe wao kwa Papa na kwa kanisa la Ulimwengu kwa ujumla, juu ya hali ya Kanisa katika taifa lao la Kenya. Na wamerudia kuonyesha ushirikiano wao kupitia fursa mbalimbali zenye kuimarisha muungano wa Kanisa Katoliki la Kenya katika umoja na Halifa wa Mtume Petro. Aidha Kardinali aliwasilisha salaam za matashi mema kwa Papa kwa niaba ya Mapadre wote , watawa wake kwa waume na waamini walei wa Kenya.Papa kwa moyo wa upendo na wa kibaba aliwapokea kwa ukarimu wote na kuwahakikishia sala zake na ukaribu wake kiroho.
Papa Francisco katika hotuba yake kwa Maaskofu wa Kenya , amegusia sehemu mbalimbali za utendaji wa Maaskofu, hasa akimtaka kila Askofu, kupanda mbegu bora ya miito kwa waumini wao, wakianzia ndani ya familia, kama shule ya kwanza ya malezi katika ubinadamu wote, na katika hitaji la vijana kutoa jibu katika miito ya kanisa. Kwa sababu hii, Papa Francisco anasema ni muhimu kwamba , nia njema za vijana wanaotaka kujiunga na seminari, hamu na bidii yao, inapaswa kusindikizwa na malezi thabiti yenye kutambua ubinadamu kwa kina , kiroho, kielimu, na huduma za kichungaji mbalimbali. Wakati huohuo Papa ameonyesha kutambua changamoto zinazowakabili katika kuimarisha juhudi hizi ,ndani ya majimbo yao , na hivyo akahimiza yote mawili kuimarisha juhudi kama Askofu binafsi na pia katika ujumla wao ili kwamba, mbegu wanayoipanda katika moyo wa Kijana iweze kuchipua kikamilifu kwa wito wa Bwana katika daraja la Upadre.
Kwa maoni hayo Papa alisisitiza kuwa , kila mmoja wao kama Askofu, anaitwa kuwa mchungaji na kama baba. Na hivyo aliwataka wawe karibu na Mapadre wao. Amesema , Mapadre wanahitaji uongozi ulio wazi na thabiti lakini wakati huohuo pia kuongozwa na huruma na hekima. Kama Maaskofu, ni lazima daima kutazama mfano wa Yesu, ambaye binafsi aliwatumikia mitume, na alitumia muda mwingi kukaa pamoja na mitume kubarizi nao. Vivyo hivyo wao Maaskofu, ni lazima wajitahidi kukaa na Mapadre wao, kuwasikiliza, kujua matatizo yao na mahitaji yao. Na pia kuwapa msaada wa kiroho unaohitajika katika kuwadumisha kama Mapadre katika uaminifu wa ahadi walizotoa na kuimarisha juhudi yao za kawaida katika kuujenga ufalme wa Mungu kwa Kenya.
Aidha Papa aliurejea Mwaka huu wa Watawa, akisema , anawakumbatia, ndani ya moyo wake, wote walio yatolea maisha yao sadaka katika kulitumikia kanisa , watawa wake kwa waume, walio yakataa ya dunia kwa ajili ya ufalme wa Mungu , ambao huleta baraka nyingi kwa Kanisa na kwa jamii ya Kenya. Papa aliwaomba Maaskofu, wafikishe salaam zake za upendo na matumaini yake kwao wote, kwamba katika mwaka huu wa Maisha yaliyowekwa wakfu, wanaweza kuushangilia kwa shangwe na ushujaa wa kumweka kwa Kristo, kuwa ngao ya maisha yao. Na kwamba wanaitwa na Kanisa kuonyesha matumaini na ushuhuda wa manufaa kwa upya wa maisha, yaliyo ahidiwa na Kristo katika Injili. Katika suala hili, Papa anasema, Kanisa lazima hasa kwa wale walio katika nafasi za uongozi na mamlaka, kusisitiza juu ya kanuni za maadili yenye kukuza manufaa ya umma na yenye kujenga ya jamii bora kwa ujumla. Katika kutimiza dhamira yake ya kitume, Kanisa lazima lichukue msimamo wake wa kinabii, kwa ajili ya utetezi kwa walio maskini na wale wanaogandamizwa na madhulumu ya rushwa zote na matumizi mabaya ya madaraka. Askofu anatakiwa kuwa mfano bora katika kuwatetea wanyonge.
Papa amewataka Maaskofu kutokuwa na woga katika hilo bali wasimame imara katika kutoa sauti ya kinabii! Na wahakikishe hekima ya Kanisa, inatambulika hasa kupitia mafundisho yake ya kijamii, na katika kuyabeba maisha ya watu wa kawaida wa Kenya. Papa alieleza na kuwahimiza Maaskofu kuimarisha viungo vyao katika huduma na ushirikiano walionao na taasisi za kidini katika taifa lao la Kenya, ili kupitia juhudi hizo , Jina la Mungu liweze kusifiwa na kutukuzwa kwa matendo ya huruma na upatanifu. Papa ameeleza na kutoa shukurani zake za dhati kwa wafanyakazi wote wanaotenda kwa unyenyekevu na ari kubwa katika taasisi za Kanisa, kwa ajili ya huduma katika yote mawili kiroho na kimwili, hasa kwa watu wahitaji zaidi. Aidha ameonyesha kufurahishwa na jinsi Kanisa linavyo changia na kuendesha shughuli zake katika maisha ya kijamii kwa manufaa ya wote, kupitia safu mbalimbali kama shule, taasisi, vyuo vikuu, zahanati, hospitali, nyumba kwa ajili ya wagonjwa na wazee, yatima na mashirika ya kijamii, ambamo Watawa hutoa mchango wao mkubwa kwa ustawi wa taifa zima. Na pia kwa ajili ya sifa ya matendo endelevu katika maisha ya sala na ibada, mihadhara, nyumba za watawa na monesteri..
Aidha Papa analihimiza Kanisa nchini Kenya daima kuuishi ukweli wa utume wake, kama chombo cha maridhiano, haki na amani. Katika uaminifu wa urithi mzima wa imani na mafundisho ya maadili ya Kanisa, waweze kuimarisha dhamira yao ya kufanya kazi na viongozi wengine , Wakristo na wasio-Wakristo katika usawa wa kukuza amani na haki katika nchi yao kwa njia ya mazungumzo, udugu na urafiki. Kwa njia hii watakuwa na uwezo wa kujenga umoja zaidi na ujasiri wa kukataa vurugu zote, hasa zinazo fanywa kwa kutumia jina la Mungu. Hili litaweza kuwapatia dhamana thabiti zaidi, kutoka kwa wananchi wote. Kwa maoni hayo Papa amesema, yuko pamoja nao ,katika sala za kuwaombea wote waliouawa katika utendaji wa kigaidi au uhasama wa kikabila au kidini katika nchi ya Kenya, na maeneo mengine ya bara la Afrika. Na kwa namna ya kipekee aliwakumbuka kafara wa ugaidi katika Chuo Kikuu cha Garissa. Wote amewaombea kupumzika kwa amani na wapendwa wao wapate faraja za Bwana na wote wanaofanya ukatili huo , waweze kuwa na hisia za ubinadamu nakuomba Huruma ya Mungu.
Papa pia, amewatia moyo Maaskofu kwa ajili ya huduma yao ya kichungaji kwa familia , hasa katika mtazamo kwamba, mwaka huu ambamo kutakuwa na Sinodi ya kawaida ya Maaskofu, kujadili suala ya maisha ya kichungaji kwa familia katika maoni ya uinjilishaji mpya. Papa ameonyesha imani yake kwa maaskofu kwamba, wataendelea kusaidia familia kubaki imara katika maisha ya ndoa , licha ya wimbi la sasa la ndoa kuvunjwa, ukafiri, madawa ya kulevya au vurugu. Amehimiza mafundisho thabiti yatolewa kwa wale wote wanaotaka kufunga ndoa , na pia kwa wale wanaopenda kujiunga katika maisha ya kitawa au Upadre. Papa anasema wote wanahitaji kufundisha ukweli kuokoa wa Injili ya Maisha.
Na hatimaye, Papa ameomba Jubilee ijao wa Huruma ya Mungu uwe ni wakati wa kutafuta msamaha kwa Bwana, wakati wa uponyaji, uongofu, na neema kwa Kanisa la zima nchini Kenya, na Afrika kwa ujumla. Na ameweka Maaskofu na Kanisa zima, chini ya Maombezi ya Mama Bikira Maria, Mama wa Kanisa, na kwa upendo mkubwa aliwapatia wote Baraka zake za Kitume.
All the contents on this site are copyrighted ©. |