2015-04-16 14:09:00

Wakristo iweni mashuhuda wa Fumbo la Ufufuko wa Kristo!


Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Pasaka Mwaka B wa Kanisa, tulialikwa kutafakari na kuishi huruma ya Mungu. Na hii itawezekana kama tukijitahidi kumfahamu Bwana. Katika Jumapili ya leo tunaalikwa  kushiriki imani pamoja na wengine. Yesu ataka wafuasi wake kuwa mashahidi na mashuhuda. Ushuhuda una pande mbili; upande mmoja – watakiwa kuona tukio, kupata ufahamu wa kitu kwa ushuhuda binafsi na siyo kusikia tu. Kwa upande mwingine – yahusisha uwezo wa kuweza kuelezea tukio hilo mbele ya wengine.

Mwaliko wa kuwa mashuhuda maana yake ni kwamba tunaitwa kwanza kuona tukio hilo halafu kushirikisha tukio hilo kwa wengine. Bahati mbaya wakristo wengi wanaishia nusu nusu tu katika ujuzi huu. Wengi hukazia kumfahamu Kristo, lakini hawako tayari kushirikisha ufahamu huo kwa wengine. Hawaishi ushuhuda wa kweli. Ndugu zangu, imani ni sawa na mshumaa uwakao – jinsi ile mshumaa huo unavyowasha mishumaa mingine, ni kiasi hicho hicho mwanga huenea. Vinginevyo mshumaa huisha na moto na mwanga wake hupotea.

Baba yake Martin Bubber, yule mwanafalsafa Myahudi aliombwa aelezee ufasaha wa mwalimu wake. Huyu baba yake Martin, alikuwa kilema wa muda mrefu. Lakini ajabu ni kwamba alipoombwa kufanya hivyo alisimama na kuanza kuelezea kwa kuruka ruka na kucheza kama alivyokuwa akifanya mwalimu wake huyo. Tangu siku hiyo akapona na ugonjwa wake wa kulemaa. Wote waliomfahamu walishangaa kweli kweli. Tunapoongea habari ya Yesu Kristo, tunafanya mambo mawili makuu. Moja – tunawasaidia wengine kumfahamuna na pili - nasi wenyewe tunapata ufahamu zaidi. Ndivyo ilivyo katika Injili ya leo.

Katika Injili ya  Lk. 24:36 – tunawasikia wafuasi wawili – baada ya kumfahamu vizuri Yesu wanarejea Yerusalemu kuwaeleza wengine lakini wanafanya hivyo baada ya kumfahamu vizuri Yesu. Katika harakati za kushirikishana imani – Yesu anatokea katikati yao. Nao wanapowaeleza wenzao kile walichokiona – nao wale wengine wakapata kuamini.

Yesu anafanya nini kwao wanaompata? Mambo mawili; kwanza, anawapatia amani yake katika mioyo yao iliyofadhaika. Halafu anajaribu kuwaonesha kwamba Yule Yesu aliyekufa kifo cha aibu msalabani ndiye aliye mbele yao. Zaidi ya hilo hata anakula chakula ili kudhihirisha anachosema. Halafu anaangazia akili zao ili kuelewa Maandiko na jinsi yanavyomwelezea. Tena anawatuma wakawe mashuhuda wake – Lk. 24,48. Ndivyo alivyofanya mbele ya mitume wake, na ndivyo anavyotokea kati yetu leo hii.

Angalia jinsi Yesu anavojishughulisha kwa ajili yetu. Ajabu kweli. Anawapa amani. Anawaimarisha imani yao na kuwaondolea wasiwasi wao. Anafungua akili zao na kuwaelezea Maandiko Matakatifu. Anawapatia ushuhuda wake. Mitume wanachofanya ni kufungua macho yao kuona, mioyo yao kupokea amani na akili zao kupokea mafundisho yake. Na anapowaambia nendeni, na wanakuwa tayari kufanya hivyo.

Ni kwa jinsi gani tunamshuhudia Kristo? Wengi wetu hawapati vyema ujumbe huu wa Kristo. Pengine njia zinazotumika siyo nzuri au sahihi katika kufikisha ujumbe huu wa Kristo mfufuka. Kadiri ya Yesu – njia ni rahisi – angalia wafuasi wawili wa Emmaus – wanaongea juu ya kukutana kwao na Kristo. Ni kuwashirikisha ni kwa nini sisi ni wakristo. Kama Mt. Petro anavyosema – 1 Pt. 3;15 – mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu, lakini kwa upole na kwa hofu.

Nasi pia tuwe tayari kuyajua mapenzi ya Mungu ili tunapoyaishi sisi, wengine wapate kumfuata. Peter Marshall anasema – mkristo si mtu anayejaribu kufanya kitu, bali ni mtu aliyepokea kitu tayari, ni mtu ambaye kuna jambo kubwa limetokea kwake, na hivyo hawezi tu kukaa kimya.

Tumsifu Yesu Kristo,

Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.