2015-04-16 13:53:00

Mambo ni magumu, Yesu anatoa darasa kwa mifano!


Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Pasaka, tunaongozwa na Injili ya Luka 24: 35-48: Yesu anaamua kutoa darasa! Hapa kuna mambo hayaendi sawa sawa! Majini, mapepo, mashetani, roho, vivuli, mizimu, viwuta, ngulyeki nk, ni majina ya viumbe visivyoonekana kwa macho ya kawaida, lakini ni viumbe vinavyotisha na kuogopesha unaposikia majina haya. Mbaya zaidi yasemekana kwamba viumbe hivyo vyaweza kuwa katika umbo lisilo la kawaida la binadamu. Mwafrika anaamini kuwa viumbe hivyo vyaweza pia kuwa ni watu walioisha kufa (marehemu) ambao wanarudi tena duniani na wanao uwezo wa kuwalinda au hata wa kuwadhuru binadamu.

Kutokana na fikra kama hizo yaonekana binadamu anao mwili tunaoweza kuuona kwa macho ya kawaida na anao pia mtima au roho isiyoonekana. Lakini mwili huo unapokufa, mtima unaweza kuchukua umbo jingine lisilo la kawaida lisiloonekana linaloweza kupenya popote hata ukutani, tena halioni njaa na wala halihitaji kula chakula kama binadamu wenye mwili huu wa kawaida. Fikra na imani kama hii walikuwa nayo pia wafuasi wa Yesu, kwamba, baada ya kufa alienda mbinguni na mwili ulio mbinguni siyo wa kawaida na hauwezi kula chakula cha kawaida tunachokula binadamu. Kwa hiyo endapo ukweli wa mwili mfufuka ni tofauti na huu mwili wetu, basi wafuasi hao walikuwa na haki kabisa kuchanganyikiwa walipomwona Yesu akiwa katika mwili wa kawaida.

Kituko hicho cha namna yake kilitokea Yerusalemu siku walipokutana wanafunzi waliotoka Emau na wale waliobaki pale Yerusalemu. Wafuasi hawa wakiwa katika kupeana taarifa za mambo yaliyomsibu Yesu aliyekufa hapo “Yesu mwenyewe alisimama katikati yao, akawaambia ‘Amani iwe kwenu.’” Ndipo wafuasi walipogutuka, “wanashtuka, wakaogopa sana, wakidhani ya kwamba wanaona roho (mzimu, pepo, jini).”

Hapa sasa ndipo tunapoingia kwenye wazo letu la kuogopa mizimu, majini, au mapepo. Yaonekana hali hii ya kushtuka na kuogopa imeandikwa ili kuelezea wazo la ufufuko, kwamba mtu aliyefufuka ni binadamu mwenye mwili wa pekee. Lakini tunachanganyikiwa tunapoletewa kinaganaga cha mwonekano wa Yesu mfufuka akiwa mtu mwenye mwili na anaongea na kula: “Akawaambia, Mbona mnafadhaika, tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe, nishikenishikeni, mwone, kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo, na walipokuwa hawajaamini kwa furaha, huku wakistaajabu, aliwaambia, mna chakula chochote? Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa. Akakitwaa, akala mbele yao.” Hapa, tunapata somo la hali ya juu kuhusu ufufuko, somo linaloelekezwa kwa wale waliozama katika fikra zinazotofautisha roho (mtima) na mwili. Ni somo muhimu zaidi hasa kwa wapagani wenye imani ya majini na mizimu.

Hapa tunaingizwa darasani na kupata somo jipya juu ya tofauti iliyopo kati ya mtu aliyefufuka na mzimu. Kwamba Yesu mfufuka siyo muzimu, wala siyo pepo. wala jini au roho. Yesu mfufuka ni mtu hai mwenye nyama na mifupa. Kuingia kwa Yesu katika ulimwengu wa kimungu hakufuti hali yake ya binadamu bali kunabadilisha tu. Hasahasa tunazinguliwa akili juu ya utata tunaokumbana nao katika kujibu maswali mengine mbalimbali ya maisha. Mathalani, tutakuwa na umbo gani tutakapoacha maisha ya ulimwengu huu? Je, tutaacha wapi mwili huu tulio nao? Je, wale waliotuacha tutaonana nao tena na kuendelea kuwapenda au kuwasamehe au kuwaomba msamaha endapo tuliwakosea? Maswali haya yanapata majibu tunapotafakari juu ya mwili wa mfufuka. Maana yake mwili mfufuka hauna mahusiano yoyote yale na mizimu, majini, pepo, bali watakaofufuliwa watakuwa na hali yao ya kibinadamu. Ndiyo maana ili kuelewesha ukweli huu mwinjili anatumia lugha ya kiyakinifu. Kama anavyosema Paulo katika barua yake ya kwanza kwa wakorinto juu ya “miili ya mbinguni, na miili ya duniani.”

Ili kulielewa vizuri wazo hilo, Yesu anatupatia mwaliko wa kutafakari mambo matatu: Mwaliko wa kwanza ni kutafakari mikono na miguu yake. “Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe.” Yaonekana Yesu alifika ulimwenguni ili kututafakarisha mikono na miguu yake. Tunakuta nguvu ya mkono wa Mungu katika Agano la kale, kwamba mkono wa Mungu ulikuwa unalipiza kisasi maadui. Huwezi kucheza na mkono wa Mungu kama asemavyo mzaburi, “Mkono wa Mungu una enzi na nguvu.” Kinyume chake mikono ya Yesu iliwashika watoto wadogo, iliwagusa wakoma, iliwashika wagonjwa, iligusa masikio ya viziwi, iligusa macho ya vipofu, iligusa ndimi zabubu na kuwaponya wote. Mikono ya Yesu iliyofanya mema ndiyo iliyopigiliwa misumari. Ndiyo maana Yesu anatualika “Tazameni au tafakarini mikono yangu.” Kadhalika anatualika kutafakari miguu yake: “Tazameni miguu yangu” iliyotembea mwendo mrefu kwa ajili ya kupenda, kwani upendo haujali urefu wa njia. Yesu alitembea kwa miguu kwa ajili ya kumpata mpendwa wake yaani binadamu ili kumpa furaha. Tunaalikwa kutafakari miguu ya Yesu na kuifuata hadi kieleweke, yaani tutafakari juu ya ulimwengu atakakotufikisha mfufuka. Kila kitu tukifanyacho, tutambue hatima yake kwamba inatupeleka wapi.

Mwaliko wa pili ni ule ambao Yesu wenyewe anaagiza apewe chakula na anachokula mbele ya wafuasi wake. Hiyo ni ni lugha ya kiyakinifu inayomaanisha kwamba ufufuko haufuti utu wa mtu na ukamilifu wake na kuugeuza kuwa pepo, la hasha, bali mtu anabaki na hali yake ya umwili lakini siyo mwili ule wa uyakinifu bali mwili mtukufu. Hapo tunaalikwa kufuta kabisa fikra za kuulinganisha mwili wa ufufuko na imani ya mapepo au mizimu.

Mwaliko wa tatu ni ule wa kusoma Maandiko Matakatifu, “ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na Maandiko,” kwa vile ni ngumu kuelewa juu ya picha hii ya mikono na miguu, na ni ngumu kuamini jinsi ya kuwatendea mema maadui, basi Maandiko matakatifu yanatufanya kuelewa lengo la Mungu juu ya ulimwengu,  kwamba katika historia daima Mungu alitaka kuonesha upendo wake kwa binadamu. Maandiko matakatifu yatakuja kueleweka vizuri zaidi ukiyasoma katika mwanga wa ufufuko na kwamba maisha ya milele yanaturuhusu kupita toka kifo na kuingia katika ulimwengu aliopitia Kristo Mfufuka. Aleluya!

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.