2015-04-14 15:06:00

Ratiba elekezi ya Papa Francisko kwa mwezi Aprili - Juni 2015


Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa Monsinyo Guido Marini, kwa idhini ya Baba Mtakatifu Francisko amechapisha ratiba elekezi ya maadhimisho ya kiliturujia yatakayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha mwezi Aprili hadi Juni 2015. Ratiba inaonesha kwamba, tarehe 26 Aprili 2015, Jumapili ya IV ya Kipindi cha Pasaka, maarufu kama Jumapili ya Kristo mchungaji mwema, Siku ya 52 ya kuombea miito mitakatifu ndani ya Kanisa, Baba Mtakatifu anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kutoa Sakramenti ya Daraja Takatifu la Upadre kwa Mashemasi walioandaliwa. Ibada hii inatarajiwa kuanza majira ya saa 3: 30 kwa saa za Ulaya.

Tarehe 3 Mei 2015, Jumapili ya V ya Kipindi cha Pasaka, Baba Mtakatifu anatarajiwa kutembelea Parokia ya “Santa Maria Regina Pacis” na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, itakayoanza majira ya saa 10: 00 za jioni. Parokia hii iko eneo la Ostia, nje kidogo ya mji wa Roma.

Tarehe 12 Mei 2015, Jumanne,  majira ya saa 11: 30 jioni, Baba Mtakatifu anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis.

Tarehe 17 Mei 2015, Jumapili ya VII ya Kipindi cha Pasaka, majira ya saa 4: 00 asubuhi, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuwatangaza wenyeheri kadhaa kuwa watakatifu, Ibada itakayoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Wenyeheri wanaotarajiwa kutangazwa kuwa watakatifu ni pamoja na: Giovanna Emilia de Villeneuve; Maria Cristina wa Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili Brabdo, Maria Alfonsina Danil Ghatta pamoja na Maria wa Yesu Msulubiwa wa Baouardy.

Tarehe 24 Mei 2015, Jumapili, Siku kuu ya Pentekoste, siku ambayo Kanisa lilizaliwa rasmi, likatoka kifua mbele kutangaza Fumbo la Pasaka, siku ya waamini walei kimataifa. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 4: 00 asubuhi. Na hapa atakuwa anaufunga rasmi mwezi Mei, uliotengwa maalum na Mama Kanisa ka Ibada kwa Bikira Maria.

Tarehe 4 Juni 2015, Alhamisi, Siku kuu ya Ekaristi Takatifu, kuanzia majira ya saa 1: 00 jioni, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu na baadaye maandamano ya Ekaristi Takatifu kutoka kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano hadi kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma. Hii ni siku ambayo wakristo wanatembea na Kristo katika viunga vya miji yao, kuonesha na kushudia uwepo wake endelevu kati ya watu wake.

Tarehe 6 Juni 2015, Baba Mtakatifu anatarajiwa kufanya hija ya kichungaji nchini Bosnia na Erzegovina ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo. Anatarajiwa kukutana na kuzungumza na viongozi wa serikali na kidiplomasia;  Baraza la Maaskofu Katoliki; viongozi wa dini mbali mbali pamoja na kukutana na vijana. Hii ni hija ya siku moja tu lakini imesheheni utajiri mkubwa wa matukio katika maisha na utume wa Kanisa nchini Bosnia na Erzegovina.

Tarehe 21 hadi tarehe 22 Juni 2015: Baba Mtakatifu atakuwa na hija ya kitume Jimbo kuu la Torino, Kaskazini mwa Italia. Huko atatembelea na kusali kwenye Sanda Takatifu, kielelezo cha mateso na mahangaiko ya mwanadamu katika nyakati zote, atashiriki katika maadhimisho ya Jubilee ya miaka 200 tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Bosco, mtume mashuhuri kwa vijana.

Tarehe 27 Juni 2015, Jumamosi, kuanzia saa 4: 00 asubuhi, Baba Mtakatifu anatarajiwa kuadhimisha Ibada ili kuridhia majina ya waamini wanaotarajiwa kutangazwa kuwa wenyeheri na watakatifu kwa siku za usoni. Tukio hili linawashirikisha kwa namna ya pekee Makardinali na viongozi wakuu wa Kanisa.

Tarehe 29 Juni 2015, Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba ya Kanisa. Kuanzia saa 3: 30, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro na kuwapatia Maaskofu wakuu Palio Takatifu watakazovishwa na Mabalozi wa Vatican kwenye majimbo yao, ili kuweza kuwashirikisha waamini kutoka katika Majimbo makuu, matendo makuu ya Mungu sanjari na kuonesha mshikamano na Maaskofu wakuu.

Kama kawaida, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itakuwa hewani kukujuza yale yatakayokuwa yanajiri katika maadhimisho haya. Lakini unaweza kupata habari kem kem za maisha na utume wa Kanisa kwa kuchungulia katika mtandao wa Radio Vatican kwa raha zako mwenyewe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.