2015-04-13 09:15:00

Shikamaneni na Askofu Sangu ili kukoleza maendeleo ya Familia ya Mungu


Askofu Liberatus Sangu amewekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu wa nne wa Jimbo Katoliki la Shinyanga na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es salaam, aliyekuwa akisaidiwa na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, na Askofu Mkuu Yuda Thaddei Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Mwanza, ambaye aliyekuwa msimamzi wa kitume wa Jimbo la Shinyanga tangu Novemba 2012 baada ya Askofu Balina kuaga dunia. Ibada hii ya misa takatifu imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mama mwenye huruma, Ngokolo, Jimboni Shinyanga, Jumapili ya huruma ya Mungu, tarehe 12 Aprili 2015.

Utume alioutenda mpaka sasa na uzoefu wake Askofu Liberatus Sangu: kuhudumia na kulipenda Kanisa, unatoa matumaini makubwa kuwa ni mtaji mkubwa na wa kutosha kuweza kuwahudumia Watu Mungu, Jimbo Katoliki la Shinyanga kwa uadilifu na upendo Mkubwa. Huo ni wosia aliopewa na Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, alipokuwa akitoa salaam za pongezi na kumkabidhi vitendea kazi vitakavyoweza kumsaidia kutenda kwa umoja na mshikamano na Maaskofu wenzake wa Baraza, ili kuleta ufanisi  na kuokoa roho za watu kwa pamoja.

Askofu Liberatus Sangu amewahi kuhudumia waamini katika Parokia za Jimbo lake Mama la Sumbawanga, amewahi kuwa mlezi wa vijana, na tangu 2008 amekuwa Afisa mwandamizi, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu.

Kwa upande wake, Askofu Mkuu Francesco Montecillo Padilla, amemkumbusha Askofu Sangu kuwa kichocheo cha imani Katoliki, maadili, kanuni, tunu za maisha na utume wa Kanisa, maendeleo na yote yanayogusa maisha ya mwanadamu katika jamii ya Shinyanga na Tanzania kwa ujumla bila kujali tofauti zao, kwani ndivyo Kristo anavyopenda wafuasi wake wamtolee ushuhuda katika Ulimwengu huu. Hivyo Askofu Sangu atapaswa kufundisha Upendo kati ya watu, kupigania haki zao hasa zinapoonekana kusetwa (kuwa hatarini, kutojaliwa), na kuhakikisha hadhi na utu wa mwanadamu unadumishwa na kuheshimiwa. Kwa mapadri, watawa na waamini wa Jimbo Katoliki la Shinyanga wanaalikwa kushikamana kikamilifu na Askofu wao mpya na kutembea naye kwa pamoja katika njia ya Msalaba, huruma na mapendo.

Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, wakati wa salaam zake za pongezi kwa Askofu Sangu, amewashukuru viongozi wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania kwa ushirikiano wao hai pamoja na serikali kwa kuwalea watu kiroho na kuwahudumia vema na kwa ubora sana katika mahitaji yao ya kijamii kama Afya na Elimu.

Amewaomba sana kuwa uhusiano huo uendelee kudumu. Ameahidi ushirikiano wa serikali katika kutafuta mema na maendeleo ya watanzania, na kwamba, wasisite kuikosoa serikali, kuwarekebisha na kuwaelekeza kwa upendo viongozi wa taifa la Tanzania. Hata hivyo ametoa angalisho hasa katika mwaka huu wa uchaguzi mkuu nchini Tanzania: kuwa baadhi ya wana siasa hupenda kujipenyeza katikati ya waamini wa imani, watu wa kabila, vyama na itikadi tofauti ili kupandikiza uchochezi uhasama wa tofauti hizo kwa ajili ya masilahi na tamaa zao za madaraka.

Rais Kikwete amewaomba viongozi wa dini nchini Tanzania kusaidia kuwaelimisha waamini wao kutoendekeza imani za kishirikina zinazopelekea mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi na vikongwe mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu pamoja na sifa ya nchi. Amesema, Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa dini ili kudumisha misingi ya haki, amani, mshikamano, utulivu na maridhiano.

Akitoa shukrani zake Askofu Liberatus Sangu aliwakumbuka wamisionari waliojituma kwa mahangaiko makubwa kuileta imani nchini Tanzania. Kwa niaba ya watanzania aliomba msamaha kwa yale mabaya waliyokutana nayo, hata kutendwa vibaya na wazawa, pengine kwa sababu mbalimbali. Amekiri kuwa vifo vyao havikuwa hitima, bali ilikuwa ni mbegu iliyopandwa ardhini nakuzaa matunda mengi na mazuri ambayo leo watanzania wananufaika nayo.

Askofu Sangu amewaalika mapadri, watawa na waamini wote wa Jimbo Katoliki la Shinyanga kumpa ushirikiano wa kutosha ili Injili isonge mbele na maendeleo ya mwanadamu yaboreke. Sumu ya maendeleo ya mwanadamu ni kuridhika, na chachu ya maendeleo hayo ni kujaribu, amefafanua Askofu Sangu.

Na Padre Celestin Nyanda,

Jimbo kuu la Mwanza.








All the contents on this site are copyrighted ©.