2015-04-06 09:26:00

Ujumbe wa Pasaka kwa Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Morogoro


Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro katika maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka ameandika ujumbe wa Pasaka kwa Familia ya Mungu Jimboni humo ambao umesomwa wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka tarehe 5 Aprili 2015. Katika ujumbe huu, Askofu Mkude anafafanua maana ya Fumbo la Pasaka katika maisha ya waamini na kwamba, Pasaka iwe ni fursa ya kuboresha maisha yao ya kiroho na kimwili sanjari na kutunza mazingira, kwa ajili ya mafao ya wengi.

Askofu Mkude anaipongeza Serikali ya Tanzania kwa kufanya maamuzi machungu ya kutoa elimu ya bure kwa wanafunzi wanaosoma kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne. Sera hii inatarajiwa kutoa unafuu kwa watanzania wengi ili kupata fursa ya elimu ambayo kimsingi ni mkombozi wa kweli Anazungumzia kuhusu Kura ya Maoni ya katiba inayopendekezwa, zoezi ambalo limesogezwa mbele hadi hapo itakapotangazwa tena kadiri ya taarifa ya vyombo vya habari.

Iwe ni fursa ya kusoma na kutoa maoni kuhusu Katiba inayopendekezwa, kwani hii ni Sheria Mama. Askofu Mkude anatoa vigezo vinavyoweza kutumiwa na Familia ya Mungu Jimboni Morogoro wakati wa kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba, 2015. Watanzania wawajibike kikamilifu katika kuchagua viongozi watakaopewa ridhaa ya kuwaongozwa watanzania kwa siku za usoni. Baada ya kukupatia kwa muhtasari yale yaliyojiri kwenye barua hii ya kichungaji, ninakuomba sasa uchakarike mwenyewe ili kuchimbua hazina na hekima iliyofichika katika barua hii ya kichungaji kutoka kwa Askofu Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro.

WAPENDWA MAPADRE,

WAPENDWA MASISTA,

WAPENDWA VIONGOZI WA VYAMA VYA KITUME,

WAPENDWA WAAMINI WAKRISTO

WAPENDWA WATU WOTE WENYE MAPENZI MEMA,

“Nawaandikia ninyi watu wa Mungu.., Jimboni Morogoro

Mlio waaminifu katika kuungana na Kristo Yesu’. (Efeso 1:1)

Nawatakieni Neema na Amani katika PASAKA HII 2015.

 

Wapendwa,

1: PASAKA NI BARAKA NA FANAKA YA MVUA NA MIMEA YETU.

Pasaka ni kipindi cha kila mwaka. Tunashangilia ushindi wa Yesu juu ya mateso na kifo, ushindi juu ya dhambi, ushindi DHIDI YA SHETANI aliyeleta duniani Dhambi ya Asili kwa kukataa kumtii Mungu Muumba Mwenyezi mwenye Upendo daima. Ndani ya Kwaresima wakati tunapojiandaa kwa PASAKA 2015 Mungu ametupatia mvua nyingi sana. HAKIKA, MVUA HUTAJIRISHA NA KUBORESHA MAZINGIRA. Naam, mvua huotesha mimea mingi na kati yao ni MIGOMBA. Ni vyema Waamini tukatambua hilo na kupanda MITI NA HATA migomba mingi zaidi NA PIA kuitunza IPASAVYO. HAKIKA, wote mnashuhudia Migomba mingi, mingi, mingi sana haituzwi: ni kama haina mwenyewe; huachwa ikue kwa kudra ya Mwenyezi Mungu na sisi wanadamu tunangojea wakati ufike tuvune ndizi za kupika au kula mbivu!!!!!!!.

 

Nawaomba sana tena sanaKatika kipindi hiki tuzitumie mvua hizi kupanda miti na migomba mingi; Aidha, TUACHANE NA KILEMA CHA ukataji wa miti OVYO. TUNAHARIBU MAZINGIRA NA KUKAUSHA VYANZO VINGI VYA MAJI. Sera yetu ya zamani ya “KATA MTI PANDA MTI” tumeizika, tuna sera mpya ya utamaduni wa kifo yaani tunaishi kwa fikra za : “KATA MTI CHOMA MTI.” Hapa naomba tuzingatie tamko la Papa wetu Francisko. Ameonya kuwa, “Mungu husamehe daima, Mwanadamu husamehe mara nyingi,  bali mazingira (nature) hayasamehi kamwe.  Tukiendelea kukakata miti ovyo, hakika hata Mkoani Morogoro tutarithi JANGWA.

 

Tunawaomba watumishi wa Serikali, wa Kilimo na Mali-Asili, watuelimishe aina inayofaa ya kilimo, miti na mazao ya kupanda katika kila kijiji kata/ Wilaya. Si kila mti unafaa kila mahali! Pasaka na hizi mvua zake vituhimize kujirudi na kujiweka upya kulingana na wakati na mahali zilipo familia zetu, ili nazo ziweze kustawi vizuri katika kila kijiji, kata na wilaya. Pasaka ituhimize tujiendeleze si tu kiroho bali pia na hata kimwili.

2. PASAKA 2015 NI BARAKA NA FANAKA KIELIMU:

Mwaka 2015 kipindi hiki cha PASAKA kinashuhudia sera mpya mintarafu ELIMU nchini mwetu. Serikali yetu imepania kutoa elimu bure hadi darasa la kumi na mbili. Huu ni uamuzi mzito na makini nasi tunaipongeza Serikali kwa ujasiri huu..  Wazazi watapata nafuu kubwa sana kwa kupunguziwa mzigo mzito wa karo ya shule. Ni matumaini yetu pia nafuu hii haitasababisha kero kwa waalimu kutopata mishahara stahiki na kwa wakati wake. Aidha Nafuu ya Ada kwa wazazi isiwe chanzo cha mafarakano kati ya Walimu na Serikali mintarafu mishahara yao, na au wanafunzi kutopata vitabu stahiki na vitendea kazi. Ikiwa hivokiwango cha Elimu nchini kitashuka mno. Tunawakumbuka tunawaombea pasaka hii. Kila la heri watumishi wa wizara ya elimu: kila la heri wanafunzi wote darasa 1 hadi 12. Hongera.

3. PASAKA 2015 NI BARAKA NA FANAKA KWA KUTOA MAONI.

Barua ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ilishauri Serikali iwape muda wa kutosha wananchi wake ili walau waelimishwe na waifahamukatiba Inayopendekezwa kabla ya kuipigia kura. Mengi yamesemwa Ushauri huo. Leo twasoma magazetini maneno kama haya; “Tunawataarifu kuwa zoezi lililotangazwa awali la Kura ya Maoni Aprili 30, 2015 limeahirishwa hadi tarehe itakayotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi baada ya kushauriana na Tume ya Taifa ya Zanzibar.”  (na Jaji Damian Lubuva, Gazeti la Raia Tanzania,  Ijumaa Aprili 30,2015 uk.1). Wapendwa Waamini, tukumbuke Neno la Mungu lasema: “ Mwenyezi Mungu asipoijenga nyumba waijengao wanajisumbua bure. Mwenyezi Mungu asipoulinda mji, waulindao wanakesha bure.” (Zab.127:1) Hii inamaanisha inatubidi tusali zaidi na kukesha mbele ya bwana kwani zoezi la katiba halijaisha ila limeahirishwa tu.

 

4. PASAKA 2015 IWE BARAKA NA FANAKA KWA UCHAGUZI MKUU.

Tusali daima kuiombea Serikali kudumisha haki na amani na uhuru wa dini. Kila mmoja wetu ana uhuru wa kumchagua mtu yeyote anayempenda au anayemwona atafaa kuwa kiongozi wetu sote, si wake yeye peke yake. Ni mtu wa staha, mchapakazi, mwungwana katika jamii au Taifa? Ni mtu wa kuaminika au mwenye msululku wa ahadi bila kutimiza. . Anawajali na kuwapenda watu wote? na hana chembe ya ubaguzi wa ukabila, udini, wa uzawa (yaani huyu wa kwetu)? Je, anawajali wanyonge, yatima, wajane, walemavu wa ngozi viziwi na wengine wenye shida mbalimbali. Ni mtu anayekuwa mkarimu hasa msimu wa uchaguzi akifyagilia kuzoa kura za wanyonge na duni.? Ni mtu wa kumwaga zawadi kwa lengo la kuwania Cheo/kiti fulani katika jamii?Taifa? Ni pia MCHA MUNGU? Hushika vyema taratibu za Dini na Imani yake au ni mtu anyepurukusha hata misingi ya Dini yake?

Naam, kura yako ni moja bali ni muhimu sana katikaUchaguzi. Ni wajibu na haki wewe ujiandikishe mapema katika daftari la wapigakura. Usikawie usizembee. Sherehekea pasaka na zingatia wajibu na haki zako kama mcha Mungu.

Nawatakia nyote neema nyingi sana Pasaka hii 2015.

ALELLUYA.

Wenu, Katika Utumishi wa YESU MFUFUKA,

+TELESPHOR MKUDE

ASKOFU WA JIMBO KATOLIKI MOROGORO. 








All the contents on this site are copyrighted ©.