2015-04-05 08:23:00

Ijumaa kuu: Msalaba ni dira na njia inayoelekea Pasaka ya Bwana!


Maadhimisho ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo yaliyoko mjini Roma, uwanja maarufu sana uliokuwa unatumika kwa ajili ya kuwashindanishia binadamu na wanyame, Ijumaa kuu, ulikuwa ni uwanja uliotumika tena kutafakari mateso na kifo cha Yesu Kristo, mambo yanayoendelea kujitokeza hata leo hii. Njia ya Msalaba iliongozwa na Baba Mtakatifu Francisko na Msalaba ukabebwa na Kardinali Agostino Vallini na waamini kutoka: Iraq, Syria, Nigeria, Misri, China na Nchi Takatifu. Haya ni baadhi ya maeneo ambayo Wakristo bado wanaendelea kunyanyasika kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kielelezo cha mwendelezo wa mateso ya Kristo hata katika ulimwengu mamboleo.

Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo kwa mwaka huu iliandaliwa na Askofu mstaafu Renato Corti wa Jimbo Katoliki Novara, Italia. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya maadhimisho ya Njia ya Msalaba aliwakumbusha waamini na mahujaji waliokuwa wamefurika kuzunguka Magofu ya Colosseo na viunga vyake kwamba, hata leo hii bado kuna Wakristo wanaoteswa na kuuwawa mbele ya macho ya walimwengu na wakati mwingine kwa kuyafumbia macho na kukaa kimya, dalili za kushiriki pia katika kuendeleza mateso haya.

Baba Mtakatifu anasema, hata leo hii bado waamini wanaendelea kushiriki katika mateso ya  Yesu Kristo kutokana na usaliti wanaoufanya kila siku, ubaya na dhambi zinazojikita moyoni na katika matendo ya mwanadamu. Katika sala hii, Baba Mtakatifu amemwomba Mwenyezi Mungu kuwakirimia waja wake msaada, neema, baraka na faraja kwa wale wote wanaotelekezwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii na familia pamoja na jamii; watu wanaobezwa na kunyanyasika kutokana na ubaguzi na hali ya kutojali utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kwamba, Misalaba yote inaonesha mateso na mahangaiko ya binadamu, lakini pia ni njia ya ufufuko, kwani Ijumaa kuu ni njia kuelekea Pasaka ya Mwanga wa Kristo, changamoto kwa waamini kutubu na kumwongokea Mungu kwa njia ya maisha na matendo. Uzito wa Fumbo la Msalaba unawasaidia waamini kupunguza uasi, ukosefu wa utii na uaminifu. Huu ndio ujumbe wa matumaini unaofumbatwa katika Fumbo la Pasaka, unaowataka waamini kumwomba Yesu Kristo neema ili aweze kuwaimarisha katika imani bila kuteteleka wakati wa vishawishi na majaribu; wawe na matumaini yasiyotindika kamwe wala kumezwa na malimwengu.

Baba Mtakatifu amesali na kuwakumbuka wakristo wote wanaoendelea kuteswa na kuuwawa kikatili sehemu mbali mbali za dunia, kama ilivyotokea Garissa nchini Kenya. Ni changamoto ya kuwa na ujasiri wa kujikita katika misingi ya upatanisho na msamaha, jambo ambalo si rahisi na linahitaji kweli neema na msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili kuweza kukumbatia upendo na huruma yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.