2015-03-28 09:04:00

Elimu ya dini isipofundishwa shuleni, taifa litachuma majanga


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linapinga wazo lililotolewa hivi karibuni nchini humo la kutaka kufuta elimu ya dini shuleni kwa kusema kwamba, ni wazo la hatari kabisa na linapaswa kubezwa kabisa kwani ni sawa na kuondoa uwepo wa Mwenyezi Mungu katika maisha ya vijana na watu wengi nchini Kenya. Jamii inayomgeuzia Mwenyezi Mungu kisogo hiyo inajitafutia majanga. Elimu ya dini shuleni haina budi kuboreshwa na kuendelezwa zaidi kama sehemu ya mchakato ya majiundo makini ya vijana wa kizazi kipya, ili waweze kuwajibika kikamilifu mbele ya Mungu na jamii inayowazunguka.

Haya yamesemwa na Askofu Maurice Muhatia Makumba, Mwenyekiti wa Tume ya elimu na dini shuleni, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika barua aliyoiandika kupinga wazo lililotolewa hivi karibuni kwenye Televisheni na Bwana Harrison Mumia aliyetaka Serikali ya Kenya kufuta elimu ya dini shuleni. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasema kwamba, Katiba ya nchi ambayo ni sheria mama inatambua uwepo na ukuu wa Mungu; inatoa fursa na haki sawa katika uhuru wa kuabudu.

Kumbe, si sawa kwa baadhi ya watu kutaka kuichanganya jamii kwa mawazo tenge ambayo yanaweza kuhatarisha tunu msingi za maisha ya kijamii, kiutu na kimaadili. Vijana wa kizazi kipya hawana budi kurithishwa tunu msingi katika medani mbali mbali za maisha, tayari kuwajibika mbele ya Mwenyezi Mungu na Jamii ya watu inayowazunguka.

Kanisa Katoliki linaamini kwamba, mafundisho ya dini na elimu bora ni mambo msingi katika mchakato wa kuwafunda vijana wa kizazi kipya mambo msingi katika maisha kwanza kabisa kama: waamini na wafanyakazi. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linaendelea kuhimiza umuhimu wa kufundisha dini katika shule, taasisi na vyuo vikuu kama sehemu ya mchakato wa majiundo makini na endelevu katika maisha ya mwanadamu anasema Askofu Maurice Muhatia Makumba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CANAA.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.