2015-03-14 15:03:00

Dhamana ya walimu katika malezi ya vijana wa kizazi kipya


Ualimu ni taaluma inayokabiliwa na matatizo na changamoto mbali mbali, lakini bado ni: kazi, dhamana na wito unaowawezesha walimu kuwaona watoto ambao wamedhaminishwa mikononi mwao, wakikua na kukomaa siku hadi siku. Kwa maneno mengine, walimu wanakuwa ni wazazi katika maisha ya kiroho, dhamana ambayo inapaswa kutekelezwa kwa dhati kabisa, ukomavu na uwiano bora zaidi wa maisha, kwa kutambua kwamba, hii pia ni dhamana shirikishi inayowahusika waalimu kama jumuiya ya walezi katika ujumla wao.

 

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 14 Machi 2015 mjini Vatican alipokutana na kuzungumza na wanachama wa Umoja wa waalimu, wafanyakazi na walezi Wakatoliki Italia, UCIIM, wakati huu wanapoadhimisha Jubilee ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwake, changamoto ya kufanya tafakari ya kina kuhusu maisha ya chama hiki katika kipindi chote hiki.

 

Ni chama ambacho kilianzishwa na Professa Gesualdo Nosengo, wakati Italia ikipambana kwenye vita kuu ya Pili ya Dunia kunako mwaka 1944. Aliona umuhimu wa kuwakusanya na kuwaunganisha walimu wakatoliki ili kushirikiana zaidi katika kuleta mabadiliko makubwa kwenye sekta ya elimu na kuwafunda kikamilifu vijana wa kizazi kipya.

 

Mambo mengi yamebadilika, lakini bado kuna waalimu ambao wanaendeleza taaluma yao kwa moyo wa dhati kabisa kwa kujikita pia katika imani na karama ambazo Mwenyezi Mungu anamkirimia mwanadamu, kwa kuonesha upendo kwa Mungu na jirani. Kwa waalimu, Baba Mtakatifu anasema, jirani zao ni wanafunzi wanaowafundisha kila siku; watu wanaosubiri mwongozo, dira na maswali na majibu katika maisha yao, changamoto ya kuwa na dhana makini ya maana ya shule inayojengeka katika mahusiano ya watu kwa kujikita katika ukarimu na wema; mambo yanayopaswa kudumishwa na wote.

 

Walimu Wakristo wanapaswa kuwapenda kwa dhati wanafunzi wao, kwa kuwa tayari kujisadaka kwa wanafunzi wenye matatizo, wanyonge na wasiobahatika, ili wao pia waweze kupata elimu bora. Walimu wawasaidie watoto watukutu, wale wasiopenda kusoma, wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi, walemavu, wageni; mambo ambayo kwa sasa ni changamoto kubwa kwa shule nyingi.

 

Waalimu wawe ni mashuhuda wa dhamana inayowasukuma kuwaendelea wanafunzi wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kuwaonesha mifano bora ya maisha ili waweze kupenda na kuthamini masomo. Walimu waoneshe umuhimu wa kusoma ili kuelimika; kujifunza ili kujenga na kudumisha mahusiano mema na wengine, ili kila mwanafunzi ajisikie kwamba, anapendwa na kusikilizwa jinsi alivyo hata katika mapungufu yake na karama zake za kibinadamu.

 

Baba Mtakatifu anasema, Kanisa limebahatika kuwa na mashuhuda wengi katika sekta ya elimu kama vile Mtakatifu Yohane Bosco, ambaye Kanisa linaadhimisha Jubilee ya Miaka 200 tangu alipozaliwa; awe ni mfano bora wa kuigwa na changamoto ya kukuza na kujiendeleza ili kweli waweze kuwa ni walimu waliokomaa na kuiva barabara. Chama hiki kilenge mbali zaidi, kwa kujikita katika mchakato wa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ujuzi na maarifa bila kusahau matumizi ya teknolojia mpya ya ufundishaji; kwa kuboresha mahusiano kati ya watu, ili kuonesha umuhimu wa shule.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.