2015-03-03 11:59:38

We, achana na Mkoa wa Mbeya!


Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema mkoa wa Mbeya unaweza kupaa kiuchumi kama utazingatia fursa za kibiashara ilizonazo na kuwekeza zaidi kwenye viwanda vya usindikaji mazao ya kilimo na mifugo. Ametoa kauli hiyo Jumatatu, Machi 2, 2015 wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Mbeya waliofika kusikiliza majumuisho ya ziara yake ya siku saba kwenye mkoa huo. Mkutano huo ulifanyika kwenye ukumbi wa Mkapa, jijini Mbeya.

“Nguvu kubwa mnayo katika biashara hasa kama mtajitahidi kutumia vema fursa kubwa ya uwekezaji katika viwanda vya kuongeza thamani kwenye mazao ya kilimo na mifugo mliyonayo,”alisema. Waziri Mkuu alisema mkoa wa Mbeya katika msimu wa 2013/2014 umeweza kuzalisha tani 4,159,907 za nafaka na kuuwezesha kuwa na ziada ya chakula ya tani 3,347,680.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema mkoa wa Mbeya bado una fursa nzuri ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara na unaweza kuiwezesha kama nchi kuuza chakula katika masoko ya Afrika na Afrika ya Mashariki kama watajipanga vizuri.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu aliwapongeza viongozi hao kwa kuuwezesha mkoa wa Mbeya kutoa mchango mkubwa katika Pato la Taifa. “Katika taarifa ya mkoa, nimeelezwa kuwa mwaka 2013, mkoa huu ulichangia shilingi trilioni 3.951 na hivyo kushika nafasi ya tatu kati ya mikoa yote nchini ikitanguliwa na mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza.”

Alisema kutokana na ukuaji wa kasi wa idadi ya watu ambao ni asilimia 2.7, mtu akichukua pato hilo la mkoa na kuligawanya kwa idadi ya watu wa mkoa wa Mbeya anapata wastani wa pato la kila mwananchi kuwa ni sh. 1,420,427. “Kipato hicho, ni sawa na shilingi 118,369 kwa mwezi au shilingi 3,946 kwa siku sawa na Dola za Kimarekani (US $) 2.3,” alifafanua.

Waziri Mkuu alibainisha kwamba mtu akichukua wastani wa pato la kila mwananchi kwa mwaka 2013 na kupanga kwa mikoa yote, mkoa wa Mbeya unashuka na kushika nafasi ya sita kitaifa. Aliitaja mikoa inayowatangulia kuwa ni Dar es Salaam sh. 1,990,043/-ambao ni wa kwa kwanza; wa pili ni Iringa (sh. 1,660,532/-); wa tatu ni Arusha (sh. 1,448,782/-); wa nne ni Kilimanjaro (sh. 1,444,882/-); wa tano ni Ruvuma (sh. 1,438,392/-) na wa sita ni Mbeya (sh. 1,420,427/-).

“Nawashauri muongeze juhudi za kuipita mikoa hiyo kwa kuwa mna fursa nyingi za kuongeza uzalishaji hasa katika mazao ya kilimo cha kahawa, kakao, mpunga, mahindi, viazi, pamoja na mazao ya maliasili kama vile mazao ya misitu, na uvuvi na uchimbaji madini,”.








All the contents on this site are copyrighted ©.